Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 23Article 543826

Habari Kuu of Wednesday, 23 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Samia awakosha Tucta, CWT

Samia awakosha Tucta, CWT Samia awakosha Tucta, CWT

VIONGOZI wa vyama vya wafanyakazi wamefurahishwa na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanza kutekeleza madai ya muda mrefu ya wafanyakazi.

Wamemuahidi kuwa watumishi watafanya kazi kwa bidii kutokana na morali mpya waliyopata.

Kauli zao zimetokana na hatua ya serikali kutangaza juzi kuwa Rais Samia amewapandisha madaraja watumishi wa umma 70,437, na watapata mshahara wa mwezi huu kulingana na madaraja waliyopandishwa, huku zikitengwa Sh bilioni 300 kuhakikisha kila anayepandishwa daraja analipwa stahiki zake.

Pia imetoa zaidi ya Sh bilioni 23 kwa ajili ya malipo ya malimbikizo ya watumishi 11,983 ambao walikuwa wakiidai serikali katika malipo mbalimbali.

Wakizungumza na HabariLEO jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Said Wamba na Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, walisema hatua ya Rais kupandisha madaraja watumishi zaidi ya 70,000 ni ishara kuwa ni msikivu na mtekelezaji.

Kaimu Katibu Mkuu wa Tucta alisema anamshukuru Rais Samia kwa kusikiliza na kuanza kutekeleza vilio vya muda mrefu vya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na madai ya wafanyakazi ya kupandishwa madaraja na mishahara.

“Tunamwomba aendelee kutusikiliza na kupokea malalamiko ya wafanyakazi na naamini huu ni mwanzo mzuri kwa watumishi wa umma, cha msingi tumpe muda kwa kuwa wavumilivu naamini atatuvusha,” alisema Wamba.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CWT amempongeza Rais Samia kutokana na uamuzi wake huo kwa sababu kitendo hicho kimeongeza furaha, amani na morali wa kufanya kazi kwa walimu na watumishi wengine kwa ujumla.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa kuna watumishi ambao wamekaa zaidi ya miaka 10 bila kupandishwa madaraja hali iliyowasababisha kukata tamaa na kushuka kwa morali ya kazi.

“Furaha ya walimu imeongezeka maradufu baada ya Mheshimiwa Rais kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa kutangaza jana (juzi) watumishi na walimu kupanda vyeo,” alisema Seif.

Alisema walimu wanamhakikishia kuwa wapo pamoja naye, wako nyuma yake watatekekeleza majukumu yao kwa moyo mmoja na kwa ufanisi wa hali ya juu.

Aliongeza kuwa kwa kuwa nusu ya watumishi wote Tanzania ni walimu, ni matumaini yake kuwa nusu ya kundi hilo watakuwa walimu.

Aliwakumbusha watumishi wote hasa walimu kuwa kupanda vyeo ni zaidi ya nyongeza ya mshahara kwa sababu unatoka daraja ulilokuwepo na kwenda daraja la juu zaidi; mfano daraja D na kuwa daraja C au daraja B au daraja A.

Kwa upande wa watumishi wa umma, Mwalimu Justine Michael wa Shule ya Sekondari Msata iliyoko wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, alisema ni jambo la faraja na la kumshukuru Rais kwa sababu kama mtumishi amekaa mda mrefu bila kupandishwa madaraja na mishahara.

Michael alisema ni kwa muda mrefu walimu wamekuwa wakipaza sauti zao kufikisha kilio chao wakitaka wapandishwe madaraja na mishahara “sasa kwa kuanza kutekelezwa na Rais Samia ni jambo la kutia moyo na kumshukuru Rais kwa kutembea katika ahadi zake.”

“Hii ni hatua muhimu sana ambayo kila mtumishi ambaye amekaa muda mrefu akitegemea atapandishwa madaraja lakini hakupandishwa kwa miaka zaidi ya mitano hadi kumi. Ni hatua ya kutia matumaini na kutufanya tujitume zaidi kazini,” alisema Michael.

Wakati akitangaza juzi kupandishwa madaraja kwa watumishi 70,437 na kulipwa malimbikizo watumishi 11,983, Mchengerwa alisema Rais Samia ameshatoa kibali cha kupandisha madaraja watumishi 91,841 hivyo watumishi wote wenye sifa ya kupandishwa madaraja watapandishwa na kupewa haki yao.