Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 11Article 584899

Habari Kuu of Tuesday, 11 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Samia awalilia 14 waliofariki ajali ya gari Simiyu

Samia awalilia 14 waliofariki ajali ya gari Simiyu Samia awalilia 14 waliofariki ajali ya gari Simiyu

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa wanahabari na wafiwa wote kutokana na ajali iliyotokea leo katika eneo la Nyamikoma wilaya ya Busega Mkoani Simiyu na kusababisha vifo vya watu 14 wakiwamo waandishi wa habari sita.

Mkuu huyo wa nchi ametuma salama hizo leo Jumaane Januari 11, 2022 akisema amestushwa na vifo hivyo vilivyotokea baada ya gari ya waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Robert Gabriel kugongana na gari ya abiria aina ya Toyota Hiace .

Katika ukurasa wake wa Tweeter Rais Samia amesema “Nimeshtushwa na vifo vya Watu 14 wakiwemo Wanahabari 6 vilivyotokea leo asubuhi baada ya gari lililokuwa katika msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kugonga na Daladala. Poleni Wafiwa, Wanahabari na jamaa wote. Mungu aziweke mahali pema roho za Marehemu na Majeruhi wapone haraka”

Mapema akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu akiwa eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Busega (DC), Gabriel Zakaria alithibitisha kutokea vifo vya watu 14 ambapo 11 walifariki papo hapo huku wengine watatu wakifariki muda mfupi baada ya ajali hiyo kutokea.

Alisema katika vifo hivyo kuna vifo vya waandishi wa habari wanne na dereva wao na watu wengine sita waliofariki papo hapo.

“Ni kweli ajali hiyo imetokea, watu 11 wamefariki kwenye eneo la tukio wakiwemo waandishi wa habari wanne na dereva na wengine sita waliokuwa kwenye gari lingine” alisema Zakaria na kuongeza.

“Dakika chache majeruhi waliopelekwa kwenye kituo cha afya cha Nasa watatu walifariki, wakiwemo wale waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyo, Blasius Chatanda alisema yupo katika hospitali ambako majeruhi walikopelekwa akiahidi kuwa atatoa taarifa baadaye huku Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel naye akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema yuko njiani kuelekea eneo la tukio.