Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 16Article 542938

Habari Kuu of Wednesday, 16 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Samia awapa mbinu vijana kupaa kiuchumi

Samia awapa mbinu vijana kupaa kiuchumi Samia awapa mbinu vijana kupaa kiuchumi

RAIS Samia Suluhu Hassan amewapa vijana mbinu za kujikwamua kiuchumi kwa kuwa vijana ni kundi lenye nguvu ya kufanya kazi na ndiyo maana wanaitwa nguvu kazi ya taifa, walinzi wa taifa, wabunifu, wana uthubutu, wajasiri na ndiyo waliobeba maono na matarajio ya taifa kwa sasa na siku zijazo.

Pia amesema uhai, usalama, maendeleo na ustawi wa taifa lolote duniani linategemea vijana kwa kuwa hakuna taifa linaloweza kusonga mbele bila kutegemea vijana.

Aliyasema hayo jana kwenye mkutano wake na vijana wote wa Tanzania kupitia vijana wa Mkoa wa Mwanza.

Rais Samia alisema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Tanzania ya mwaka 2012, katika kila watu 10, wanne ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35, lakini kiuhalisia hadi miaka 50 bado ni vijana na kwa sasa Tanzania ina vijana milioni 20.7 na asilimia 11.4 ya vijana wenye uwezo wa kufanya kazi hawana ajira.

Kutokana na wingi na umuhimu wao kwa taifa, Rais Samia aliwapa mbinu vijana za kujikwamua kiuchumi kwa kutumia fursa zilizopo kikiwemo kilimo, ufugaji na uvuvi.

Alisema Tanzania ina jumla ya hekta milioni 29 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambako vijana wanaweza kujiajiri. Alisema sambamba na kilimo, vijana pia wanaweza kujiajiri kwa kujikita kwenye usambazaji wa pembejeo na zana za kilimo, huduma za ugani, biashara na masoko, usafirishaji, usindikaji mazao na fursa nyingine nyingi.

“Jitihada za serikali pekee haziwezi kumaliza matatizo ya vijana, ni lazima ninyi vijana wenyewe muwe mstari wa mbele. Natoa wito kwenu kutumia fursa zilizopo. Kwenye mifugo, Tanzania ni wa pili Afrika kwa kuwa ni mifugo mingi, pia tuna eneo la maji lenye ukubwa wa kilometa za mraba 397,937 sawa na asilimia 41.1 ya eneo lote la Tanzania ambalo linafaa kwa uvuvi, vijana mnajipangaje kwenye eneo hili, hizi zote ni fursa” alisema.

Fursa nyingine ni uchumi wa mtandao ambako serikali imewekeza fedha nyingi kwenye Mkongo wa Taifa na Kituo cha Kanzidata.

Aliwaambia vijana kuwa kinachotakiwa ni kujiamini na kutumia fursa hiyo kwa kuwa kwenye mtandao kuna fursa pana kwa vijana kujiajiri, lakini cha kusikitisha vijana wengi wanatumia mitandao vibaya kwa kulaumu na kushutumu, badala ya kuitumia kimaendeleo.

Mbinu nyingine aliyowapa vijana kujikwamua kiuchumi ni kushirikiana ili wafikie malengo yao badala ya kila mmoja kufanya mambo peke yake.

Alisema wanaposhirikiana inakuwa rahisi pia kwa serikali kuwasaidia na kuahidi kuendelea kuwapa ushirikiano vijana wajasiriamali na wabunifu walioanzisha biashara kupitia umoja wao wa TSA.

“Ushiriki wenu vijana wa Tanzania kwenye mambo yanayohusu vijana kwenye Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mataifa (UN). Mnashiriki vipi vijana wa Tanzania? Hilo nalo vijana mnatakiwa kulifanyia kazi, vinginevyo mkubali kunyang’anywa haki zenu na hamjui wapi mnaelekea,” alisisitiza.

Rais Samia pia aliwataka vijana kuijua sera yao ya mwaka 2007 ili waifanyie marekebisho kukidhi matarajio yao kwa kuwa kuna mabadiliko makubwa yametokea hapa nchini na duniani ambayo yameathiri sera hiyo.

Eneo jingine ambalo aliwataka vijana kujikita kama sehemu ya kujikwamua kiuchumi ni sanaa na utamaduni ambako kuna ajira nyingi.

Alisema kwa miaka ya hivi karibuni sekta hiyo imekuwa ikukuwa kwa kasi na kutoa ajira nyingi kupitia michezo mbalimbali, muziki na filamu na kuwaahidi kuanzia Desemba mwaka huu wasanii wataanza kulipwa mirabaha yao kwa kazi zinatumiwa kwenye redio, televisheni na mitandao.

Kutokana na serikali kuboresha upatikanaji wa umeme, Rais Samia aliwataka vijana kuutumia umeme kama fursa ya kukuza uchumi wao kwa kujiajiri katika mambo mbalimbali.

Pia alisema serikali imejenga mazingira mazuri kwenye sekta binafsi ili wenye mitaji wajiajiri ikiwemo kufuta tozo kwenye mifugo, uvuvi na kilimo, upatikanaji wa leseni kwa urahisi na kufuta kodi kero ili kuwapa vijana wepesi wa kujiajiri.

“Kwenye madini tumefuta tozo na kodi mbalimbali na kutenga maeneo ya wachimbaji wadogo yenye ukubwa wa hekta 38,567. Maeneo mengine ambako tumeboresha mazingira ili kuongeza fursa za ajira kwa vijana ni kwenye sekta ya utalii ambako tumeanzisha hifadhi mpya tano za kitaifa, tumenunua ndege mpya 11 na kupunguza ada ya leseni ya biashara ya utalii kwa wakala wa kusafirisha watalii wenye magari chini ya manne kutoka dola za Marekani 2,000 hadi dola 500,” alifafanua Rais Samia.

Alisema serikali pia inatekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR), Bwawa la Kufua umeme la Julius Nyerere, Daraja la Magufuli Mwanza, ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini

Uganda hadi Tanga ambayo vijana wanaweza kuchangamkia fursa za ajira zilizopo.

Pamoja na kuwapa vijana mbinu za kujiajiri, Rais Samia pia alisema serikali yake itaendelea kutoa mafunzo ya ujuzi ili vijana wajiajiri pamoja na kushughulikia changamoto zao mbalimbali ikiwemo ya kukosa maeneo ya kufanyia shughuli zao.