Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 22Article 543712

Habari Kuu of Tuesday, 22 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Sekondari 310 kujengwa mwaka ujao wa fedha

SERIKALI imetenga Sh bilioni 220 katika mwaka wa fedha 2021/22 kujenga shule za sekondari za kutwa 310 kati ya 1,000 zinazotakiwa kujengwa nchini.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde, alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Anastazia Wambura, aliyetaka kujua kama Mkoa wa Mtwara wenye kata 57 zisizo na shule za kata zitajengewa shule hizo katika mwaka huu wa fedha.

Silinde alisema serikali imepanga kujenga shule 310 katika mwaka huu wa fedha na kwamba, itaendelea kujenga shule hizo katika miaka ya fedha inayokuja hadi zitakapokalimisha shule 1,000.

Silinde alisema kwa sasa kuna kata 780 zisizo na shule za sekondari za kutwa nchini na zote zitajengewa hata katika kata zenye wanafunzi wengi, zitajengwa shule nyingine za kata ili kupunguza idadi ya wanafunzi waliorundikana katika shule moja.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge Wambura aliyetaka kujua ni lini ujenzi wa shule za sekondari utaanza katika kata zisizo na shule za sekondari nchini ili kuendana na mpango wa serikali wa kuhakikisha kila kata inakuwa na shule ya sekondari.

Silinde alisema serikali kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari, itajenga shule mpya 1,000 za sekondari za kutwa nchini kwa kuanza na ujenzi wa shule za sekondari kwa kata zote azisizo na shule za sekondari.

Mradi huo unatakelezwa kwa awamu na katika mwaka wa fedha 2021/22, serikali imetenga Sh bilioni 220 kujenga shule 310 mpya za sekondari za kutwa nchini.