Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 11Article 542164

xxxxxxxxxxx of Friday, 11 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Sekta ya mifugo yayumba

SEKTA ya mifugo ikiwamo ng’ombe na mbuzi imeyumba kwa kiasi kikubwa kutokana na kukosekana maeneo ya kutosha ya malisho ya wanyama hao.

Hayo yalisemwa na Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk Khalid Salum Mohamed wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini, Machano Othman Said(CCM) aliyetaka kujua mikakati ya serikali ya kuimarisha sekta ya ufugaji na kuzalisha maziwa.

Dk Mohamed alizitaja sababu za kuyumba kwa sekta hiyo ni kukosekana kwa maeneo ya malisho ya mifugo pamoja na maeneo mengi kutumika kwa shughuli za ujenzi wa nyumba za kudumu.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni ukosefu wa mbegu bora za ng’ombe wa kisasa ambao ni maarufu kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa.

Aidha, alisema wizi wa mifugo ni miongoni mwa changamoto zilizojitokeza hivi karibuni ambapo wafugaji wengi wameanza kukata tamaa na maendeleo ya sekta hiyo.

Aliyataja maeneo ya Magharibi A ambayo awali yalikuwa yakitumika kwa ajili ya malisho ya wanyama hivi sasa yamegeuzwa kuwa makazi ya watu.

“Ni kweli sekta ya ufugaji hivi sasa imeyumba sana kutokana na maeneo mengi ya malisho kutumika kwa shughuli za ujenzi wa nyumba za kudumu,'' alisema.

Aliitaja mikakati ya baadaye ya serikali ni kujenga kiwanda cha malisho ya chakula cha mifugo ambacho kwa kiasi kikubwa kitaimarisha sekta ya ufugaji.

Join our Newsletter