Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 26Article 574126

Habari Kuu of Friday, 26 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Sekta ya uvuvi yachangia 1.7% Pato la Taifa

Uvuvi wachangia 1.7% Pato la Taifa Uvuvi wachangia 1.7% Pato la Taifa

Shughuli za uvuvi na maisha ya wavuvi wadogo nchini zimeongezeka katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru, huku sekta hiyo ikichangia Pato la Taifa kwa asilimia 1.7.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki wakati akielezea mafanikio ya sekta ya mifugo na uvuvi katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru.

Alisema katika kipindi cha mwaka 1961 – 1988 shughuli za uvuvi katika maeneo yote ya uvuvi nchini zilikuwa zikifanywa na wavuvi wadogo huku kiasi cha samaki kilichozalishwa na wavuvi wadogo kutoka kwenye maji asili kimeongezeka kutoka tani 385,771.80 zenye thamani ya Sh bilioni 7.73 mwaka 1986 hadi tani 473,592.24 zenye thamani ya Sh trilioni 2.36 mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 18.54.

Ndaki alisema baada ya uhuru, wavuvi wadogo waliendelea kutumia zana duni za uvuvi ambapo takribani asilimia 80 ya vyombo vyote vya uvuvi vilikuwa vikitumia kasia kama nyenzo.

Alisema mwaka 1987, kati vyombo 6,667 vilivyokuwa vikifanya shughuli zake katika Ziwa Victoria, ni 172 vilivyokuwa vikitumia injini za kisasa ikilinganishwa na mwaka 2008 kati ya vyombo vya uvuvi 58,231, vyombo 8,191 vilikuwa vikitumia mashine za kisasa, idadi hii imeendelea kuongozeka hadi kufikia 13,593 mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 65.

Alisema kumekuwapo na ongezeko la idadi ya wavuvi, vyombo vya uvuvi na kiasi cha samaki kilichovunwa kuanzia mwaka 1995, ambapo idadi ya wavuvi ilikuwa 75,621, vyombo vya uvuvi 22,976 na kiasi cha tani 255,900.74 za samaki zenye thamani ya Sh 70,467,575.96 zilivunwa ikilinganishwa na idadi ya wavuvi 195,435 waliotumia vyombo 58,231 na kuvuna tani 473,592.24 za samaki zenye thamani ya Sh 2,367,961,211.36 mwaka 2020.

Alisema katika kuimarisha ubora wa mazao ya uvuvi katika mnyororo wa thamani, serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya uvuvi ikiwamo ujenzi na ukarabati wa mialo ya kupokelea samaki na masoko. Alisema hadi sasa kuna jumla ya mialo ya kisasa 33 na masoko 17 ikilinganishwa na mwaka 1961 ambapo hapakuwa na mialo iliyoboreshwa na masoko ya kisasa.

“Kufuatia juhudi hizo kiasi cha mazao ya uvuvi yanayouzwa nje ya nchi yameendelea kuongezeka kutoka tani 17,269.90 na samaki wa mapambo 4,116 zenye thamani ya Sh bilioni 11.93 mwaka 1995 hadi tani 40,477.97 na samaki wa mapambo 128,316 zenye thamani ya Sh bilioni 386.37 mwaka 2020.”

“Aidha, mauzo hayo yaliingizia taifa Sh milioni 629.57 mwaka 1995 ikilinganishwa na Sh bilioni 21.67 mwaka 2020 kama mrahaba,” alisema.