Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 24Article 573814

Habari Kuu of Wednesday, 24 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Serikali: Matapeli wa ajira kukiona cha moto

Serikali yaandaa mfumo kudhibiti matapeli wa ajira Serikali yaandaa mfumo kudhibiti matapeli wa ajira

Serikali inaandaa mfumo wa kielektroniki wa huduma za ajira utakaowezesha vijana wanaotafuta ajira ndani na nje ya nchi kuhudumiwa kwa ufanisi ili kudhibiti mawakala wanaopeleka Watanzania nje kiholela.

Akizungumza jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amesema hatua hiyo ni katika kuhakikisha Watanzania wanaounganishiwa kazi nje ya nchi wanakuwa salama.

Jenista amesema mwaka 2018, serikali ilipiga marufuku watu kupelekwa nje kufanya kazi kutokana na ukiukwaji wa taratibu huku baadhi ya kampuni zikiwa feki.

Amesema kama kuna Mtanzania alipelekwa nje ya nchi kufanya kazi kuanzia mwaka 2018 hadi sasa hakwenda kihalali.

Jenista amesema Sheria ya mwaka 1999 ilikuwa inaelekeleza kampuni ambayo imepata kibali kutoka Ofisi ya Kamishna wa Kazi ya kuunganisha Watanzania huduma za ajira nchi za nje kuhakikisha kila robo mwaka inatoa mrejesho kuhusu wanafanya kazi gani wamepelekwa, mikataba yao ikoje na inaisha lini, jambo ambalo lilikuwa halifanyiki

"Nilipiga marufuku utaratibu wa kuunganishwa wafanyakazi na fursa za ajira nje ya nchi baada ya kufanya utafiti na kubaini utaratibu mzima unakwenda kinyume kwani kampuni zingine zilikuwa feki, hazijasajiliwa," amesema.

Ameongeza; "Kutokana na hilo tumefanya maamuzi ikiwemo muongozo mpya ambao utaziwajibisha kampuni ambazo ni wakala wa huduma za ajira nchi nzima ambao watakwenda kinyume, kwani mwongozo unaonyesha wanatakiwa kufanya nini katika kuwaunganisha Watanzania na masoko ya ajira ya nje."

Jenista amesema kupitia mwongozo mpya kwa sasa wataruhusu kupeleka wafanyakazi kwenye nchi ambazo Serikali imeingia mkataba wa makubaliano ya kutaka wafanyakazi.

"Nilikuwa nasema Tanzania tunakwama wapi, kwa nini tusiwapeleke wenye ujuzi? Kama tunawapekeka wasichana kwenda kufanya kazi za ndani nje ya nchi kwa nini wasipate mafunzo VETA ili tukiwapeleka wanakuwa wamepata mafunzo na wana cheti. Akienda akiwa na cheti ataheshimika lakini unampolepeka hana ujuzi, hana cheti ni rahisi sana kunyanyasika na kuingia katika maisha hatarishi," amesema.

“Tukitumia utaratibu huu wafanyakazi wetu watakuwa salama," alisema.

Ameongeza kusema kuwa serikali inaanzisha utaratibu wa kufanyia upembuzi wa kina kampuni ambazo ni wakala wa huduma za ajira ili kujua unandani wao.