Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 28Article 540247

xxxxxxxxxxx of Friday, 28 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali haina mpango wa kuwawezesha wanaume

SERIKALI haina mpango wa kuanzisha utaratibu wa kuwawezesha kiuchumi wanaume.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk Festo Dugange wakati wa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo (CCM).

Mbunge huyo alitaka kujua ni nini mpango wa serikali kuwawezesha wanaume kiuchumi baada ya mpango wa halmashauri kuwawezesha wanawake, vijana na wenye ulemavu kuonesha mafanikio makubwa.

Akijibu, Dk Dugange alisema kwa sasa mamlaka za serikali za mitaa zinaendelea na utaratibu wa kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Mikopo hiyo hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 Kifungu cha 37A inayoelekeza halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato inayokusanya kwa ajili ya mikopo ya asilimia nne kwa wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.

“Lengo la mikopo hii ni kusaidia makundi maalumu katika jamii ambayo hayawezi kupata kirahisi mikopo katika benki za biashara na taasisi za fedha kwa sababu ya masharti magumu ikiwamo dhamana na riba kubwa,” alisema.

Dk Dugange alisema serikali imetoa kipaumbele kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa kutokana na wengi wao

hawakopesheki katika benki na taasisi za fedha.

“Kwa sasa serikali haikusudii kuanzisha mpango wa kuwawezesha wanaume au akinababa,” alisema.

Akiuliza swali la nyongeza, Tarimo alihoji kama serikali haioni haja ya kuongeza umri wa vijana wanaonufaika na mikopo hiyo kufikia miaka 45 ili wengine hususani wakina baba wanufaike na mikopo hiyo.

Dk Dugange alisema katika mikopo hiyo inatolewa kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 35 na kwamba serikali bado haijawa na mpango wa kuongeza umri.

“Kwa sasa tutaendelea kutekeleza sheria hii wakati tunatathimini uwezekano wa kuongeza umri,” alisema.

Join our Newsletter