Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 23Article 559309

Habari za Afya of Thursday, 23 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali imeanza mchakato wa kupunguza gharama za kusafisha damu na vipimo

Serikali imeanza mchakato wa kupunguza gharama za kusafisha damu na vipimo Serikali imeanza mchakato wa kupunguza gharama za kusafisha damu na vipimo

MKURUGENZI Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Dk Gabriel Mhidze, amesema gharama za kusafisha damu kwa wenye matatizo ya figo maarufu dayalisisi, zitashuka hadi chini ya Sh 100,000.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Maelezo TV, jijini hapa, Dk Mhidze alisema kwa sasa gharama za huduma hizo ni kati ya Sh 250,000 na Sh 300,000, hali inayowashinda watu wengi.

Alisema MSD imeingia mkataba na moja ya viwanda vya kuzalisha mashine za huduma za dayalisisi baada ya kukuta zinauzwa kwa bei nafuu zaidi na kwamba, wameahidiwa na watengenezaji hao kupunguziwa bei zaidi kama wataagiza mashine nyingi.

Dk Mhidze alisema kwa sasa wao MSD wamepanga bei ya huduma hizo za dayalisisi zishuke hadi Sh 100,000 au chini yake.

"Tumepanga mashine hizo ziwe na bei ndogo zaidi ili kituo cha afya hata kilichopo Tandahimba kitoe huduma ya dayalisisi kwa 100,000 au chini yake," alisema.

Mkurugenzi huyo MDS alisema kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NIHF), watavikopesha vituo hivyo mashine hizo ambazo awali zile kubwa zilikuwa zikiuzwa Sh milioni 150, lakini sasa wanatarajia kuzinunua kwa Sh milioni 55.

Aidha, alisema mashine zilizokuwa zikiuzwa kwa Sh milioni 57, zitauzwa kwa kati ya Sh milioni 25 na 27, huku zilizokuwa zikiuzwa milioni 27 sasa zitauzwa kwa Sh milioni 14. Mashine zilizokuwa zikiuzwa kwa Sh milioni 14 zitauzwa kwa Sh milioni saba wakati zile za milioni saba, zitauzwa kwa Sh milioni mbili.

Huduma za dayalisisi hufanyika pale figo za mtu zinaposhindwa kufanya kazi ya kuchuja uchafu na maji yasiyohitajika mwilini na hivyo kuwa njia bandia kwa mwenye tatizo hilo.