Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 30Article 560617

Habari Kuu of Thursday, 30 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali imepandisha madaraja watumishi 180,0000

Serikali imepandisha madaraja watumishi 180,0000 Serikali imepandisha madaraja watumishi 180,0000

SERIKALI katika kipindi cha mwaka mmoja imepandisha madaraja watumishi wake 180,000; jambo ambalo halijawahi kutokea katika miaka ya nyuma. Aidha kuna kibali cha kuajiri watumishi 46,000 na waliajiriwa 10,000 na bado kuna nafasi 36,000.

Kibali cha kuajiri watumishi 36,000 wa serikali bado kinafanyiwa kazi na hivi karibuni zitatangazwa nafasi 1,200 za ajira kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kauli hiyo imetolewa na Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mohammed Mchengerwa wakati akifungua mkutano wa watendaji wa wakala za serikali mjini hapa.

Idadi iliyopandishwa madaraja ni mara mbili iliyoelezwa na serikali Aprili mwaka huu, kupitia Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.

Katika mkutano huo alisema serikali inatarajia kupandisha madaraja watumishi wa umma 90,000 nchi nzima lengo likiwa ni kutimiza takwa la kisheria linalotaka watumishi waliokidhi vigezo kupandishwa madaraja.

Pamoja na kueleza upandishaji huo, Waziri Mchengerwa pia ameagiza maofisa utumishi ambao hawakuwasilisha taarifa za watumishi ili wapandishwe madaraja wawajibishwe.

Alisema maofisa hao hawafai kuwepo kwenye nafasi walipo hivyo wataondolewa na kurudishwa wizarani ili wapangiwe kazi nyingine.

“Nawaagiza kwenda kuangalia taasisi ambayo ililegalega kuleta taarifa za watumishi wapande madaraja, Rais anajua nguvu ya serikali ni watumishi wa umma, maofisa utumishi ambao hawakufanya vizuri tuweze kuwaondoa na kupeleka watu wengine kwa ajili ya kufanya kazi hiyo”alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu ajira mpya Mchengerwa alisema:”Wizara ilishapata kibali cha kuajiri watumishi, muende kuangalia ajira ya vibarua au mikataba msitengeneze mwanya wa watumishi hewa,” alisema Mchengerwa.

Aliwataka kila wakala utangaze kazi inazofanya na watimize wajibu wao ipasavyo ili kuongeza tija na serikali ipate mapato.

Mchengerwa pia alitaka ipelekwe orodha ya wanaokaimu nafasi kwa muda mrefu ili ipelekwe kwenye mamlaka husika.

Pia alitaka utazamwe uwezekano wa kuhamisha watumishi kwenye eneo la ununuzi ili wakaone yanayoendelea kwenye taasisi nyingine.

“Maofisa manunuzi wengine ukiwahamisha wajumbe wa bodi wanakuja kukulalamikia hapo sasa utaona lazima kuna kitu kinaendelea,” alisema Mchengerwa.

Pia aliwataka watendaji hao wazingatie sheria na taratibu zilizopo kwenye utekelezaji wa miradi ya kimkakati na akasema serikali inataka miradi hiyo ikamilike kwa wakati.

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome alizitaka taasisi hizo ziboreshe huduma na kuoneza wigo wa mapato ya ndani ili kuipunguzia serikali mzigo.