Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 12Article 551212

Habari za Afya of Thursday, 12 August 2021

Chanzo: MWANANCHI

Serikali kuanza kutoka kadi za "Kielektroniki" kwa wanaochanja

Wananchi wakipokea kadi maalum za Kielektroniki Wananchi wakipokea kadi maalum za Kielektroniki

Serikali imeanza kutoa kadi maalum za kielektroniki zenye vigezo vya kimataifa vya uthibitisho wa kuchanjwa chanjo ya ugonjwa wa Covid 19 zitakazoitwa Vaccine Electronic Certificates.

Shughuli hiyo imeanza leo Alhamisi Agosti 12, 2021 katika ukumbi wa Karimjee ambapo wanahabari, wasanii na watu mbalimbali wamejitokeza kupata chanjo hiyo.

Kadi hizo zenye QR Code zina vigezo vya kimataifa ikiwemo kuwa na utambulisho wa siri ambao itajumuisha taarifa za mpokeaji chanjo, chanjo aliyopata, muda na mahali alipochanjwa.

Katibu mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi amesema kwa wale ambao walichanjwa na kupata kadi ya kawaida kuanzia wiki ijayo watapigiwa simu na kupatiwa kadi za kielekitroniki baada ya kujiridhisha kupitia taarifa za wizara.

Profesa Makubi amesema Serikali inatoa tahadhari iwapo kuna watu watakaojaribu kujipatia vyeti hivyo kwa njia za udanganyifu, kuwa watabainiwa na mfumo na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Wizara inafahamu mfuatano wa namba zake na zimetolewa kituo gani hivyo ikitokea namba moja imejirudia uchunguzi utaanzia kwa watoa huduma waliotoa namba hizo na wateja wenye vyeti vya namba hizo.

“Ntoa wito kwa watoa huduma ya chanjo na wapokea huduma za chanjo kila mmoja kutimiza wajibu wake na kujiepusha na udanganyifu wowote,"amesema.

Kaimu mkurugenzi Tehama wa Wizara ya Afya, Silvanus Ilomo amesema mfumo huo ni wa uhakika na hakuna namna ya kufoji vyeti na hata wale waliochanjwa wanatakiwa kurejesha kadi za mwanzo na watapatiwa vyeti vyenye QR Code.

“Mfumo uliotumika kutengeneza cheti hiki kila utakapokwenda duniani kinaonyesha kimetengenezwa na Wizara ya Afya Tanzania."

“Tutaanza hilo zoezi vituo vyote nchini wakichanja watapata hivi vyeti nasisitiza tusijaribu kufoji kwa sababu taarifa zote tunazo kwenye database na zina reference namba ukifoji haitaonekana,” amesema Ilomo.

Mganga mkuu wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Elizabeth Nyema amesema watatoa huduma ya kuchanja katika ukumbi wa Karimjee leo na kesho na kwamba mpaka mchana walishachanja watu 150.