Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 12Article 551185

Habari za Mikoani of Thursday, 12 August 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Serikali kutoa bilioni 35 uwanja wa ndege Musoma

Maboresho Uwanja wa Ndege Musoma Maboresho Uwanja wa Ndege Musoma

Serikali imesema inatarajia kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 35 kuboresha uwanja wa ndege wa Musoma, mkoani Mara, kwa kuweka lami na kuongeza urefu wa uwanja huo ili kuruhusu ndege kubwa na ndogo kuweza kutua.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, alipofika uwanjani hapo kukagua maandalizi ya ujenzi huo.

“Tunatarajia ujenzi huu utagharimu shilingi Bilioni 35 ambapo utahusisha upanuzi wa uwanja huu na pia uwekaji wa lami, naamini kazi hizi zikikamilika uwanja huu utakuwa wa kisasa zaidi”, amesema Chamuriho.

Aidha,Waziri Chamuriho, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo na vitongoji vyake ambao watapata ajira katika mradi huo, kuhakikisha kuwa wanatumia vizuri fursa watakayoipata kwa kuwa waaminifu na kufanya kazi kwa bidii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Khalfani Haule, amesema kuwa mradi huo ukikamilika utarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Musoma na pia kuchochea biashara ya utalii kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ipo mkoani humo.

Ameongeza kuwa Uongozi wa Wilaya tayari umejipanga kwa kuupokea mradi huo na wameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mkandarasi huyo kwa kumpatia eneo la kuchimba mchanga na kokoto za ujenzi.