Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 15Article 547045

Habari za Afya of Thursday, 15 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali kutoa chanjo 4 za corona

Serikali kutoa chanjo 4 za corona Serikali kutoa chanjo 4 za corona

SERIKALI imeagiza zaidi ya aina nne za chanjo ya kujikinga na corona na zinatarajiwa kuanza kutumika ndani ya miezi mitatu au minne au kabla ya hapo.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi alisema jana serikali imeagiza zaidi ha aina moja ya chanjo ili wananchi wawe na uhuru wa kuchagua watumie ipi.

Profesa Makubi alisema maambukizi ya corona yapo kwenye mikoa mbalimbali ila hali si mbaya, lakini wananchi waendelee kuchukua tahadhari.

“Kwa hiyo watu watakuwa na option ya kuamua mimi nachukua hii, nachukua hii, kwa hiyo kama mambo yataenda vizuri ndani ya miezi mitatu au minne ijayo tutakuwa tumeanza kupata chanjo,” alisema alipozungumza kwenye kipindi cha Morning Trumpet kilichorushwa na chaneli ya U Tv ya Azam Media.

Profesa Makubi alisema aina chanjo hazitofautiani sana katika uwezo wa kuzuia maambukizi ya virusi vya corona na kwamba wana taarifa baadhi ya makundi yameanza kupata kinga hiyo Zanzibar.

Alisema serikali imeagiza chanjo kutekeleza miongoni mwa mapendekezo 19 ya wataalamu wa Kamati ya Corona iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Profesa Makubi alisema mgonjwa wa kwanza wa Covid-19 alipatikana nchini Machi 16, mwaka jana na kwa mujibu wa takwimu za jana, hadi sasa watu milioni 180 wameugua na milioni nne kati ya hao wamefariki duniani.

Alisema uzoefu unaonesha kuwa kiwango cha maambukizi kimekuwa kikiongezeka katika miezi ya Januari, Aprili na Julai, na chanjo zikifika kuna makundi yatapewa kipaumbele wakiwemo watumishi katika sekta ya afya na wasafiri.

Alisema Rais Samia ameruhusu ofisi za ubalozi zitoe chanjo na kwamba serikali imetoa mwongozo kusimamia hilo.

“Na tumetoa jana (juzi) mwongozo una-guide jinsi gani ya wao kuingiza chanjo na sisi kuratibu na kuziangalia zimeingia ngapi, nani kachomwa na anaendeaje baada ya kuchomwa,” alisema Katibu Mkuu Afya.

Profesa Makubi aliwataka wananchi waepuke misongamano isiyokuwa ya lazima hasa kwenye baa, mikutano ya siasa na hata kumbi za muziki ili kuepuka kuambukizwa virusi vya corona.

Alisema miongozo mbalimbali inayoendelea kutolewa na serikali ni lazima kufuatwa ili kukabiliana na ugonjwa huo huku akiwataka wanaougua corona kujitahidi kuepuka hofu ili wapone kwa haraka na kuendelea na ujenzi wa taifa.

Alisema serikali kwa upande wake imekuwa ikiendelea kukabiliana na kusambaa kwa maambukizi hasa katika kuhakikisha mipango yake inatekelezwa kwa ufanisi huku akiwataka wafanyakazi waliopewa majukumu mbalimbali katika kudhibiti corona kutimiza majukumu hayo kwa wakati.

Alisema katika kukabiliana na ugonjwa huo, serikali imeweka uwakilishi kutoka kila sekta inayohusiana na ugonjwa huo moja kwa moja au hata isiyohusika moja kwa moja.