Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 28Article 540262

xxxxxxxxxxx ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali kutoa tamko kuhusu matumizi ya ‘Force Account’

SERIKALI imeahidi kutoa tamko kuhusu utaratibu unaotumiwa kufanya kazi za ujenzi bila kutumia makandarasi maarufu kama Force Account, ambao unalalamikiwa na makandarasi.

Imesema itatoa tamko hilo Juni, mwaka huu kwenye mkutano wa mashauriano baina ya Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na wadau wa sekta ya ujenzi utakaofanyika mkoani Mwanza.

Ahadi hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Leonard Chamuriho wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa mashauriano wa wadau wa sekta ya ujenzi ulioandaliwa na CRB.

“Serikali inalifanyia kazi suala hilo na hata Mwenyekiti wa Bodi ya CRB amelizungumza hapa, muwe wavumilivu tutalitolea tamko Juni mwaka huu kwenye mkutano wa nne utakaofanyika mkoani Mwanza,” alisema.

Waziri huyo alisema hayo baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi, Consolatha Ngimbwa kumweleza kuwa utaratibu huo umesababisha maumivu makubwa kwa wakandarasi wa ndani kwani kwa muda mrefu hawana kazi.

Ngimbwa alisema mwaka 2018 serikali iliamua kutumia utaratibu huo ikisema wakandarasi wa ndani wamekuwa wakitoza fedha nyingi ambazo haziendani na miradi husika, hivyo kulazimika kutekeleza miradi yake yenyewe ili kuokoa fedha nyingi.

“Makandarasi wameshajifunza na wako tayari kufanya kazi kwa bei ya chini na kwa ubora wa hali ya juu kwani wameshapewa mafunzo ya mara kwa mara na CRB na kwa sasa wameiva kufanya kazi hizo.”

“Baada ya serikali kuanza utaratibu wa Force Account kwa maelezo kuwa bei za wakandarasi wa ndani ni kubwa, tuliwapa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu namna ya kujaza zabuni, tulikwenda mikoa mbalimbali na kwa kweli wameiva na wako tayari kufanya kazi za serikali,” alisema.

Chamuriho aliwataka makandarasi kuwafichua maofisa wa serikali ambao wamekuwa wakiwaomba rushwa ili wawape zabuni mbalimbali za ujenzi.

“Mkandarasi anapopewa mradi kwa kutoa rushwa mara nyingi miradi haikamiliki kwa wakati na wakati mwingine inafanywa kwa viwango vya chini, hivyo kuwakosesha wananchi haki zao.”

“Huu ni wakati mwafaka kwa wakandarasi wazalendo kuungana na kutumia fursa zilizopo kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi kwa kuweka ubinafsi pembeni,” alisema.

Chamuriho alisema kazi nyingi za ujenzi zinafanywa na kampuni za nje kutokana na wakandarasi wa ndani kukosa uwezo wa mitaji, mitambo ya kutosha na rasilimali watu, hivyo kuungana ndiyo itakuwa suluhisho la matatizo yao.

“Serikali haifurahii kuona kandarasi kubwa zinafanywa na kampuni za nje, acheni ubinafsi muungane mpate uwezo wa kuzifanya nyinyi kwa sababu mkizifanya nyinyi gharama itashuka na fedha zitabaki nchini,” alisema.

Join our Newsletter