Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 19Article 572701

Habari Kuu of Friday, 19 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Serikali kuwabana wanaorithishana nyuma za TBA kinyemela

Serikali kuwabana wanaorithishana nyuma za TBA kinyemela Serikali kuwabana wanaorithishana nyuma za TBA kinyemela

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara ametaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuboresha mikataba ya wapangaji kuondokana na changamoto ya baadhi ya watu kuachia mtu nyumba kinyemela.

Waitara alisema hayo jijini hapa wakati wa kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi miwili ya nyumba 20 za viongozi zinazojengwa eneo la Kisasa na nyumba 150 za watumishi wa serikali zinazojengwa eneo la Nzuguni.

Alisema kuna haja sasa kwa TBA kuangalia namna ya kuboresha mikataba ili kumbana mpangaji kutoa ukazi wa nyumba za wakala kiholela badala yake, alazimike kurudisha taarifa serikalini. Waitara alisema kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa nyumba za TBA hazitumiki ipasavyo.

Mengine ni kuhusu tatizo la watu kuachiana nyumba bila kufuata utaratibu. “Ule utaratibu wa mpangaji muda wake wa upangaji ukiisha na kutakiwa kuhama nyumba za TBA, badala ya kurudisha nyumba anaamua kumuachia mtu mwingine kimyakimya uachwe, na ili kuondokana na hili tuboreshe mikataba ya upangaji,” alisema.

Aidha, Waitara aliagiza wakala kujenga nyumba zaidi ya 150 kwa kiwango na wahakikishe wanakamilisha kwa wakati ujenzi wake ili kuwezesha watumishi kupanga. Alisisitiza kuwa hatarajii visingizio vya kuchelewa kukamilika miradi kwa sababu vifaa vya ujenzi vinapatikana.

Akizungumzia mradi wa nyumba 20 za viongozi, Mkadiriaji Majenzi wa TBA, Goddy Mduda alisema kati ya nyumba hizo zilizojengwa asilimia 50 zipo katika hatua ya kumalizia. Wakati huohuo, Waitara ameagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha wanashughulikia madai ya kuwapo dalili za kudaiwa rushwa kwa vijana wanaoomba kufanya kazi kwenye mradi wa barabara ya mzunguko katika Jiji la Dodoma yenye kilometa 112.3.

“Nimetumiwa meseji kuwa wakati mnachukua vijana kufanya kazi hapa kuna malalamiko yanatolewa kuwa kuna dalili za rushwa ili wapate kazi, hivyo sisi serikali hatutaki kusikia hilo, lifanyieni kazi hili maana linachafua taswira ya serikali na wakala wenyewe,” alisema.

“Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza wananchi wanaozunguka miradi inayotekelezwa wapewe kazi kama wana vigezo bila kuzungushwa, sasa kukianza maneno maneno ya kuwa wanadaiwa rushwa linakuwa si jambo jema na kama lipo basi tabia hii iachwe na mnaosimamia hili fanyeni kazi kwa weledi na kutoa kazi kwa wananchi.”

Alisema serikali inatekeleza mradi wa barabara za mzunguko kutokana na kuwa na manufaa makubwa kiuchumi na itapunguza msongamano katika Jiji la Dodoma.

“Kulikuwa na upotoshaji kuwa mradi huu hautatekelezwa, sasa mmeshalipwa asilimia 20 ya fedha hadi sasa hivyo chapeni kazi kwa mujibu wa mkataba ambao unaeleza hadi Desemba 7, 2024 uwe umekamilika hivyo mkiweza malizeni hata kabla ya muda,” alisema.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dodoma, Leonard Chimagu alisema mradi huo ulianza Septemba mwaka huu na utatekelezwa ndani ya miezi 79. Alisema Sh bilioni 12.47 zimelipwa kama fidia kwa wananchi 2,388 waliopisha mradi na kati ya hao, 470 waliobaki wanaendelea kulipwa sababu fedha zimeshatolewa wiki iliyopita.