Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 06Article 541255

Habari Kuu of Sunday, 6 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali mbele kwa mbele

Serikali mbele kwa mbele Serikali mbele kwa mbele

IKIWA ni siku 78 tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoapa kuongoza nchi, serikali imeeleza inavyotekeleza mambo mbalimbali, miongoni mwake ikiwa ni maendeleo mazuri ya miradi ya kimkakati ambayo mpaka sasa imepatiwa Sh trilioni 2.6.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dodoma kwamba, kuazia Machi 19 mwaka huu tangu Samia awe Rais, kila kitu kinakwenda vizuri na Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza majukumu yake vizuri ya kuongoza nchi.

“Leo (jana) ni siku kama 80 hivi tangu tuondokewe na aliyekuwa rais, John Magufuli…tumwombee… pia ni siku 78 tangu mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aingie madarakani akiwa rais katika awamu ya sita,” alisema.

Alisema utoaji wa fedha katika miradi hiyo ya kimkakati ni kuendeleza kuimarisha misingi ya uchumi wa nchi. Alisema mazungumzo yanaendelea kwa miradi mipya kupeleka nguvu katika uchumi wa viwanda.

Alisema kuanzia Machi mwaka huu mpaka sasa, mikataba ya Sh bilioni 845 imeshasainiwa na mikataba ya Sh trilioni 2.6 iko njiani kusainiwa hivi karibuni. Baada ya mikataba kukamilika, miradi yote hiyo itakuwa na thamani ya Sh trilioni 3.5.

“Miradi inaendekea kutekelezwa na fedha zinakwenda kufanya kazi kama ilivyopangwa” alisema.

Miradi ya kimkakati Akizungumzia ujenzi wa Reli ya Kisasa,SGR, Msigwa alisema ujenzi wa kutoka Dar es Salaam – Morogoro (kilometa 300) umefikia asilimia 91, Morogoro – Makutupora (km 422) umefikia asilimia 61 na ujenzi wa reli ya Mwanza – Isaka umeanza na serikali imetoa Sh bilioni 372.34 za ujenzi wa kilometa 341 za reli hiyo.

Kuhusu Bwawa la Julius Nyerere katika mto Rufiji, ujenzi umefikia asilimia 52 kutoka asilimia 45. Kwa upande wa ununuzi wa ndege, alisema ndege tatu mpya zitawasili wakati wowote na kukamilisha idadi ya 11 zilizokusudiwa.

Akizungumzia mradi wa ujenzi wa Daraja la Kigongo– Busisi mkoani Mwanza, utakaogharimu Sh bilioni 712 hadi kukamilika kwake Februari, 2024 alisema sasa umefikia asilimia 27.

Upande wa miundombinu ya Dar es Salaam,alisema daraja la Tanzanite limefikia asilimia

77.19 wakati madaraja ya juu ya Chang’ombe na Kurasini, BRT 2 (barabara ya Kilwa), DMDP, upanuzi wa barabara ya Morogoro, kazi zinaendelea na zipo katika hatua nzuri.

“Ujenzi wa Meli MvMwanza (Hapa Kazi Tu) umefikia asilimia 74 Na katika mwaka wa huu kuna mikataba tisa ambapo ujenzi wa meli mpya tatu zitajengwa katika maziwa makuu, meli mpya moja katika Bahari ya Hindi. Pia kutakuwa na ukarabati wa meli tano katika maziwa ya Victoria na Tanganyika,” alisema Msigwa.

Uchumi mzuri Akizungumzia hali ya uchumi kwa ujumla, alisema ni nzuri japo madhara ya covid 19 kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani yamesababisha kuyumba kwa uchumi.

“ Uchumi wetu uliokuwa unakua kwa wastani wa asilimia 6.9 umeshuka kidogo hadi wastani wa asilimia

4.7, na matarajio ni kuwa uchumi wetu utaendelea kukua vizuri kutokana na hatua madhubuti ambazo zimechukuliwa,” alisema na kuongeza kuwa mfumuko wa bei kwa sasa ni wastani wa asilimia 3.3 ambayo ni kiasi kizuri.

Ukusanyaji mapato

Akiba ya fedha za kigeni alisema ni nzuri, zinatosha kununua bidhaa na huduma kwa muda wa zaidi ya miezi 4.7.

Sekta Binafsi Alisema ili kuimarisha ukuaji wa uchumi, Serikali ya Awamu ya Sita imekutana na watu wa Sekta binafsi wakiwa ni wadau muhimu kwa kuwa ni injini ya uchumi inayozalisha ajira na kustawisha wananchi huku ikilipatia pato taifa.

Alisema ni nia ya Rais Samia kuona sekta binafsi inaimarika kwa kuondoa vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi, unyanyasaji dhidi ya wafanyabiasha na kujenga miundombinu inayohitajika.

“Kumekuwa na matokeo mazuri sana juu ya uamuzi huu, wafanyabiashara na wawekezaji wengi wameanza kuimarisha biashara zao na kuleta uwekezaji mbalimbali. Wote mmeona hivi karibuni mfanyabiashara Aliko Dangote amekutana na Mheshimiwa Rais na wamezungumza kuhusu uwekezaji wake hapa nchini,” alisema.

Dangote ana kiwanda cha saruji Mtwara ambako amewekeza Dola milioni 770 sawa na Sh trilioni 1.761, na sasa anataka kuwekeza kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbolea.

Pia Msigwa alisema serikali ina dhamira ya kuhakikisha kwamba Sekta Binafsi haiendi hovyo, ikivunja sheria kwa kukwepa kodi bali itoe mchango wake inavyotakiwa kwa manufaa ya nchi .

Kujali wamachinga

“Na kwa kukutana na wafanyabiashara hawa, haina maana kwamba Serikali sasa imeamua kuwatelekeza wafanyabiashara wadogo (Machinga, Mama Lishe) wote mmeona juzi tu Rais alikuwa Soko la Kariakoo ambako amejionea mazingira ya wafanyabiashara wadogo na ameahidi kufanyia kazi changamoto zinazowakabili,” alisema Msigwa.

Alisema serikali itawalinda na hakuna namna yoyote ambayo inaweza kutowajali. “Rais ni mama na angependa familia ziwe na amani, wafanyabiashara wadogo wawe na amani wahakikishe wanafanya kwa kufuata taratibu na miongozo,” alisema.

Ukusanyaji mapato

Akizungumzia ukusanyaji wa mapato, alisema Rais anawapongeza Watanzania wote kwa kuitikia mwito wa kulipa kodi, akisema makusanyo yanaendelea vizuri.

Alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kurekebisha dosari zilizokuwepo katika ukusanyaji wa kodi kistaarabu baada ya maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia.

Alifafanua kwamba vikosi kazi ambavyo vilitumika kukusanya kodi katika baadhi ya maeneo, vimeondolewa na Watanzania wanalipa kwa utaratibu wa kawaida kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Msigwa alisema ingawa yapo maeneo mengi kuhusu suala la ulipaji kodi kwa utaratibu, alisema TRA wameagizwa kukusanya kodi na watu hawakuambiwa wasilipe kodi.

“Hapa napo pamekuwa na maneno mengi, wengine wanaona kama vile maelekezo ya Mheshimiwa Rais yanatoa mwanya wa watu kutolipa kodi, Hapana. Ulipaji wa Kodi unaendelea kwa mujibu wa Sheria, … hakuagiza watu wasilipe kodi na wala hajasema TRA wasikusanye kodi. Alichokipiga marufuku ni ukusanyaji wa kodi wa kutumia mabavu, vitisho na kuharibu biashara za wafanyabiashara,” alisema.

Alisema katika kuonesha uwapo wa maendeleo mazuri ya ukusanyaji kodi, msemaji huyo wa serikali alitoa takwimu na kusema

kutolewa kwa maelekezo, matokeo yamekuwa mazuri.

Mwenendo wa Makusanyo ya Kodi kuanzia Januari mpaka Machi mwaka huu unaonesha, Januari malengo yalikuwa Sh trilioni 1.68 na makusanyo ni Sh trilioni 1.34 sawa na asilimia 79.8

Februari malengo yalikuwa Sh trilioni 1.61, makusanyo Sh trilioni 1.33 sawa na asilimia 82.9. Machi malengo yalikuwa Sh trilioni 1.99 na makusanyo ni Sh trilioni 1.67 sawa na asilimia 84.1.

Malengo ya makusanyo kwa Aprili ilikuwa Sh trilioni

1.61 na makusanyo ni Sh trilioni 1.34 sawa na asilimia 83.2. Aprili malengo ni kukusanya Sh trilioni 1.619 na makusanyo ni Sh trilioni 1.33 sawa na asilimia 82.

“Kwa hiyo Watanzania msiwe na hofu, Serikali inakusanya kodi kama kawaida kwa ajili ya kuendesha shughuli zake na kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo kugharimia mishahara, kuhudumia deni la Taifa, kugharamia miradi ya maendeleo” alisema Msigwa.

Bandari safi Akizungumzia Bandari ya Dar es Salaam kama lango kuu la uchumi, alisema ufanyaji kazi umeongezeka, idadi ya meli zinazoingia zimeongezeka na mapato yamekua.

Alitoa mfano wa Aprili kwamba mapato yalikuwa Sh bilioni 73.2 huku Mei ni Sh bilioni 84.6 kiwango alichosema kilikuwa kikubwa ikilinganishwa na mapato ya Machi ya Sh bilioni 80.2.

Join our Newsletter