Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 11Article 542197

Habari Kuu ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali yaanika mafanikio ya bajeti

Serikali yaanika mafanikio ya bajeti Serikali yaanika mafanikio ya bajeti

SERIKALI imeeleza mafanikio na changamoto za bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021.

Akisoma hotuba ya mapendekezo ya bajeti ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 bungeni, Dodoma jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema serikali ilipanga kukusanya jumla ya Sh trilioni 34.88 kutoka katika vyanzo vyote vya ndani na nje na kwamba hadi kufikia Aprili, mwaka huu na Sh trilioni 24.53 zilikuwa zmekusanywa sawa na asilimia 86.1 ya lengo la kipindi hicho.

Akitoa mchanganuo wa fedha hizo, alisema mapato yaliyokusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalifikia Sh trilioni 14.54, sawa na asilimia

86.9, mapato yasiyo ya kodi yalifikia Sh trilioni 1.80 sawa na asilimia 78.5 ya lengo na mapato yanayotokana na vyanzo vya ndani vya mamlaka za serikali za mitaa yalifikia Sh bilioni 607.4 sawa na asilimia 88.5 ya lengo.

Alisema misaada na mikopo nafuu iliyopokelewa ilikuwa Sh trilioni 1.89 sawa na asilimia 70.4 ya lengo, mikopo ya ndani ikijumuisha ya kulipa dhamana za serikali zilizoiva ilifikia Sh trilioni 3.99 sawa na asilimia 95.7 ya lengo na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara ilifikia Sh trilioni 1.68 sawa na asilimia 88.1 ya lengo.

Akizungumzia athari za mlipuko wa ugonjwa covid-19 kwenye uchumi kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Mwiguli alisema umesababisha kutofikiwa kwa baadhi ya malengo ya makusanyo ya mapato ya ndani.

Alizitaja sekta zilizoathiriwa zaidi za mlipuko wa ugonjwa huo na kushusha mapato ni, utalii, usafiri wa anga na uingizaji wa bidhaa kutoka nje.

Aidha, alisema baadhi ya mashirika na taasisi zimeathiriwa na covid-19 na hivyo kupungua kwa michango na gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

“Mathalani, mapato ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania yameathiriwa kufuatia kuporomoka kwa shughuli za utalii kulikosababishwa na kusambaa kwa Uviko-19 (covid-19) katika nchi zinazoleta watalii wengi nchini,” alisema.

Hata hivyo, alisema katika kuhakikisha lengo la mapato ya ndani linafikiwa, serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kama ilivyoainishwa ndani ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na Kufanya Biashara Nchini (Blueprint) kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi.

“Serikali pia imeendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji sahihi wa sheria, kanuni na taratibu za kodi, kuboresha mifumo ya Tehama ikiwamo Electronic Fiscal Device Management System (EFDMS),” alisema.

“Misaada na mikopo nafuu iliyopokelewa hadi Aprili 2021 ni Sh trilioni 1.89 ikilinganishwa na Sh trilioni 1.82 mwaka 2019/20. Pamoja na athari za mlipuko wa uviko-19, misaada na mikopo nafuu iliongezeka kwa asilimia 3.84 ikilinganishwa na kiasi kilichopokelewa katika kipindi kama hicho mwaka 2019/20,” alisema.

Join our Newsletter