Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 29Article 560254

Habari za Afya of Wednesday, 29 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali yaipatia Sekou Toure bil 1/- za dawa

Serikali yaipatia Sekou Toure bil 1/- za dawa Serikali yaipatia Sekou Toure bil 1/- za dawa

HOSPITALI ya Rufaa Sekou Toure mkoani Mwanza, imepokea zaidi ya Sh bilioni moja kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba, hivyo kuwezesha upatikanaji wa dawa za kutosha kwa mahitaji ya wagonjwa.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou Toure, Dk Bahati Msaki jana jijini Mwanza alipokuwa akizungumza na HabariLEO. Alisema fedha hizo zimetolewa na serikali ili kuwezesha kununua dawa kwenye Bohari ya Dawa (MSD).

Alisema wamepokea fedha hizo zaidi ya wiki moja iliyopita na kwa sasa hospitali hiyo haina tena changamoto ya upatikanaji wa dawa, hivyo wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi mbalimbali wanapata dawa bila kikwazo.

Dk Msaki aliwaomba wagonjwa wanaotumia Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF) ambao wamekuwa hawapati dawa katika vituo vya zahanati kwenda vituo vya afya na hospitali za wilaya na wanapokosa baadhi ya huduma kufika katika hospitali ya rufaa ili wapate dawa ambazo hawakupata.

Alisema katika kuhakikisha kuwa kuna uhakika wa upatikanaji wa dawa, wamefungua duka jingine hivyo alisema uwepo wa milango mingi ya utoaji wa dawa itawasaidia wagonjwa.

Dk Msaki alisema kuwa kuwepo kwa mfumo wa ulipiaji wa fedha za matibabu kwa wakati unaofanywa na mifuko mbalimbali ya bima ya afya pamoja na wagonjwa wanaolipia fedha taslimu unawezesha kuwepo kwa fedha za kutosheleza ununuzi wa dawa.