Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 22Article 543667

Habari Kuu of Tuesday, 22 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali yakusanya trilion 6/- kupitia NMB kidigiti

Serikali yakusanya trilion 6/- kupitia NMB kidigiti Serikali yakusanya trilion 6/- kupitia NMB kidigiti

SERIKALI imekusanya mapato yenye thamani ya Sh trilioni sita kupitia benki ya NMB kwa mifumo ya kisasa hasa ya kidijitali katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2018.

Mifumo hiyo pia inatajwa kuwa na mchango mkubwa katika ufanisi wa benki hiyo kifedha.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alimwambia Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango mwishoni mwa wiki mkoani hapa kuwa, ubora wa benki hiyo kiutendaji katika miaka ya karibuni na mafanikio yake kifedha mwaka jana, ni miongoni mwa matokeo ya ubunifu na uwekezaji katika mifumo ya kisasa hasa ya kidijiti.

Alimwambia Dk Mpango kuwa, mifumo hiyo imekuwa na tija kubwa si tu kwa taasisi hiyo, bali pia kwa serikali, wananchi na uchumi wa taifa kwa jumla.

Zaipuna aliyasema hayo kabla ya kukabidhi hundi ya Sh bilioni 21.8 kwa Makamu wa Rais zilizotolewa na NMB kwa serikali kama gawio la mwaka 2020 likiwa ni ongezeko la asilimia 43 ya kiasi ilichokitoa mwaka 2019.

“Pamoja na miradi hii, uwekezaji ambao Benki ya NMB imeufanya kwenye teknolojia, unaendelea kuiwezesha benki kuunganisha mifumo yake na taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali na hivyo, kurahisisha ukusanyaji wa mapato,” alisema.

Akaongeza: “Mbali na Serikali kuwa mbia, pia ni mteja mzuri na mkubwa wa NMB. Tunalitambua hilo na tumeendelea kuwekeza katika teknolojia inayotoa suluhisho kwa serikali.”

Katika hafla hiyo, Dk Mpango alisema mbali na malipo ya gawio la Sh bilioni 155.8 lililotolewa na NMB kwa serikali katika kipindi cha zaidi ya miaka 10, mchango mwingine mkubwa wa NMB ni kuiwezesha serikali kukusanya mapato kupitia mifumo yake.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, serikali inajivunia mafanikio makubwa ya NMB na kuwa kwake mbia katika taasisi hiyo hali inayoifanya kupata faida nyingi zenye tija kutokana na uwekezaji wake wa asilimia 31.8.

“Tunajivunia uwekezaji wetu katika NMB kwani unalipa. Serikali kwa niaba ya wananchi tunaipongeza NMB kwa kazi inazozifanya kuwahudunmia Watanzania na uchumi wa taifa kwa uumla,” alisema Dk Mpango.

Katika kipindi cha miaka mitano, benki hiyo imekuza mtaji wa wanahisa wake kwa ongezeko la zaidi ya Sh bilioni 463, hivyo kuufanya mtaji wake kufikia Sh trilioni 1.1 ukilinganisha na Sh bilioni 666 mwaka 2015.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Dk Edwin Mhede alisema zaidi ya ubunifu wa kidijiti, siri kubwa ya mafanikio ni wafanyakazi ambao ndio silaha ya benki hiyo.

Mpaka Desemba mwaka jana, Benki ya NMB ilikuwa na akaunti za wateja zaidi ya milioni nne na mawakala zaidi ya 8,400 waliotapakaa nchi nzima.

Michezo

Biashara

Burudani

Afrika

Maoni