Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 21Article 573283

Habari za Mikoani of Sunday, 21 November 2021

Chanzo: mwananchidigital

Serikali yamaliza utata kijiji kinachogombewa na halmashauri mbili Tanga

Serikali yamaliza utata kijiji kinachogombewa na halmashauri mbili Tanga Serikali yamaliza utata kijiji kinachogombewa na halmashauri mbili Tanga

Serikali kupitia Msajili wa Vijiji imefuta hati zote zilizokuwa zinatambulika mwanzo na badala yake imetoa hati mpya ya usajili inayotambua kuwa Kijiji cha Bumba chenye vitongoji nane kipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Mkoani Tanga.

Hati hiyo ya usajili imekuja baada ya kuwepo na mvutano kati ya Halmashauri ya Bumbuli na Korogwe ambapo kila halmashauri ikidai kijiji hicho kipo katika eneo lake baada ya eneo hilo kugundulika kuwa madini ya zilicon.

Kwa Mujibu wa hati hiyo iliyosainiwa na Msajili wa Vijiji kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Dk Charles Mhina imethibitisha kuwa kuanzia tarehe 5/4/1975 Kijiji hicho kimesajiliwa katika halmashauri Bumbuli.

Vitongoji nane vilivyotajwa kuunda Kijiji hicho ni; Chumbageni, Dara, Elemu, Gare, Mlama, Pwai, Kwebamba na Mtae ambapo ofisi za Serikali ya Kijiji hicho itakuwa Kitongoji cha Elemu.

"Kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 22 na 26 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) sura 287 natangaza Kijiji cha Bumba Kiko katika halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli na kwa maana hiyo inafuta hati zote zilizokuwa zimetolewa kabla” Amesema Msajili huyo wa Vijiji kutoka Makao Makuu ya nchi Dodoma.

Akisoma hati hiyo mbele ya mamia ya Wananchi wa Kijiji hicho, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Kalisti Lazaro amesema kuwa yeye na wananchi hao wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapatia hati ya kijiji hicho na kwamba mambo mengine kama ramani ya kuonyesha mipaka wataendelea kufuatilia ili nayo ipatikane hatimaye wajue mipaka yao .

Mkuu wa Wilaya huyo amesema kuwa vijiji vyenye migogoro lazima visajiliwe kisheria na pamoja na mambo yote muhimu lazima izingatiwe pia senteni ya mwisho iliyosema "Kuwa hati hii inafuta hati zote zilizotolewa awali"

Ameongeza kuwa kwa sheria ya ardhi na sheria ya Vijiji ili muwe na mamlaka ya ndani ya kijiji chenu ni lazima kijiji kisajiliwe na kiwe na hati, na kwamba kwa hati hiyo waliyopewa inawafanya kuwa mamlaka kamili na kwasasa kinachotakiwa ni wao kuhakikisha wanapanga matumizi bora ya ardhi.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema suala la ramani na mipaka ni jambo dogo kubwa ilikuwa ni kupata hati kwanza halafu hayo mengine yatafuatwa.

"Nitawaomba mbunge wetu, January Makamba na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava tufanye kikao cha pamoja ili tuzungumzi suala zima la mashamba yalikuwa yanalimwa upande huu na upande ule" amesema Kalisti

Ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani nikosa kisheria, kauli yake hiyo imekuja baada ya wananchi kumlalamikia kwamba wananchi wa Korogwe wanawapiga na kuwanyang’anya vifaa vyao wakidai eneo hilo la mashamba ni lao hivyo watu wa Bumbu hawaruhusiwi kulima.

Wananchi wa Kijiji hicho wameishukuru Serikali kwa kuwapatia hati hiyo ambayo inawafanya wabaki kuwa katika halmashauri ya Bumbuli.

Mzee Athuman Akida (76) amesema mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu umekwisha huku akitoa shukrani kwa Mbunge wao na Mkuu wa Wilaya kwakuamua kupambana ili kupata suluhisho ikiwemo kupata hati hiyo.

Hata hivyo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Hozza Mandia ameipongeza Serikali na kwamba kilichobaki ni kujikita kwenye shughuli za maendeleo pamoja na kupanga matumizi bora ya ardhi.