Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 03Article 540757

xxxxxxxxxxx ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali yaokoa bilioni 320/- mafuta bandarini

SERIKALI inaokoa Sh bilioni 320 kwa mwaka kutokana na mfumo wa kusimamia mpangilio wa meli zinazoleta mafuta nchini. Pia inaokoa Sh bilioni 360 kwa mwaka kutokana na mfumo wa kuagiza mafuta kwa pamoja.

Hayo yalielezwa bungeni jana na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Katika mwaka wa fedha 2021/2022, wizara hiyo inakadiria kutumia Sh trilioni 2.386 ikilinganishwa na Sh trilioni 2.197 iliyotengwa kwa mwaka 2020/21, sawa na ongezeko la asilimia nane.

Alisema serikali kupitia Bodi ya Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) imeendelea kusimamia mpangilio wa meli zinazoleta mafuta nchini ili kupunguza siku za meli kusubiri kushusha mafuta kutoka katika meli ambapo wastani wa siku za kusubiri kwa sasa ni tano ikilinganishwa na wastani wa siku 75 mwaka 2015.

“Gharama za demurrage zimepungua kutoka wastani wa dola za Marekani 45 kwa tani hadi wastani wa dola za Marekani 3.6 kwa tani kutokana na siku za meli kusubiri kushusha mafuta kupungua. Kwa tathmini hii, mfumo huu unaokoa takribani shilingi bilioni 320 kwa mwaka zilizokuwa zinatumika kulipia demurrage,” alisema.

Alisema Serikali kupitia PBPA imeendelea kusimamia Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja ambapo gharama za uletaji mafuta zimeendelea kuwa na wastani wa dola za Marekani 36 kwa tani ikilinganishwa na dola za Marekani 83 kwa tani mwaka 2015 kabla ya mfumo huu kuanza na hivyo kuokoa wastani wa Sh

bilioni 360 kila mwaka.

Alisema kiasi cha gesi ya mitungi (LPG) kinachoingizwa nchini kimeendelea kuongezeka ambapo kwa mwaka 2020, kiasi kilichoingizwa kwa ajili ya matumizi ya hapa nchini na nchi jirani ni tani 194,597 ikilinganishwa na tani 166,436 zilizoingizwa mwaka 2019, sawa na ongezeko la asilimia 16.92.

“Matumizi ya ndani ya gesi yameongezeka hadi kufikia tani 121,834 mwaka 2020 ikilinganishwa na tani 106,301 mwaka 2019, sawa na ongezeko la asilimia 14.61.

“Ongezeko hilo limechangiwa na juhudi mbalimbali za Serikali kwa kushirikiana na kampuni zinazouza LPG katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutumia LPG katika kutunza mazingira na kupunguza madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi ya kuni na mkaa,” alisema.

Kuhusu mwenendo wa bei za mafuta, Dk Kalemani alisema kwa miezi kumi na moja ya mwaka 2020/21, wastani wa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia ilikuwa dola za Marekani 52.96 kwa pipa, sawa na pungufu ya asilimia 0.5 ikilinganishwa na wastani wa dola za Marekani 53.22 kwa pipa kwa kipindi kama hicho katika mwaka 2019/20.

“Bei ya mafuta ghafi katika soko la Dunia ilishuka mwaka 2020/21 kwa sababu matumizi ya mafuta duniani yalipungua kutokana na kupungua au kisimamishwa kwa shughuli za kiuchumi katika nchi mbalimbali duniani ikiwa ni hatua zilizochukuliwa na nchi hizo kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona,” alisema

Alisema katika mwaka ujao wa fedha wamelenga kutekeleza miradi ya umeme mikubwa ya kimkakati ukiwamo wa Julius Nyerere (megawati 2,115), Ruhudji (megawati 358) na Rumakali (megawati 222).

Join our Newsletter