Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 24Article 559384

Habari za Afya of Friday, 24 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali yaombwa kuongeza mashine za kupima usikivu

Serikali yaombwa kuongeza  mashine za kupima usikivu Serikali yaombwa kuongeza mashine za kupima usikivu

MWENYEKITI wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (Shivyawata) mkoani Shinyanga, Richard Mpongo, ameiomba serikali kuongeza mashine za upimaji usikivu kwa viziwi walioko shuleni na walimu maalumu wenye kufundisha lugha ya alama.

Mpongo aliyasema hayo jana mjini Shinyanga wakati wa maadhimisho ya siku ya lugha ya alama duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Mwanza, ambapo aliwataka wazazi kuwaanzisha shule ya awali watoto viziwi ili waweze kufahamu lugha ya alama mapema.

Mpongo ambaye pia ni mwalimu mstaafu wa elimu maalumu, alisema serikali inataka watoto wote viziwi wenye umri wa kwenda shule wapelekwe shule ili wajifunze alama ya lugha kwa maendeleo yao na kuwepo walimu maalumu kwa ajili yao.

"Walimu waliopo wenye kufundisha lugha ya alama hawatoshi hivyo naomba serikali iajiri walimu maalumu wa kutosha na kwenye shule za kawaida walimu wenye taaluma hiyo watolewe na badala yake wapelekwe kwenye shule ambazo zina watoto wenye uhitaji wa lugha ya alama," alisema.

Mwalimu wa lugha ya alama shule maalumu ya msingi Buhangija iliyopo Manispaa ya Shinyanga, Rose Daudi, alisema watoto wa darasa la awali na darasa la kwanza bado wana changamoto katika uelewaji wao kwa sababu mashine za kupimia usikivu zimekuwa chakavu.

Daudi alisema watoto hao hawapati lugha ya alama kiufasaha kutokana na uhaba wa walimu kwani kuna jumla ya walimu watano na upungufu ni walimu tisa.

Alisema watoto viziwi wamekuwa wakiletwa kuanza shule wakiwa na umri wa miaka mitano na mpaka sasa kuna wanafunzi 30 wa darasa la awali na la kwanza lakini hawana mwalimu maalumu wa kuwafundisha.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha viziwi mkoani Shinyanga (CHAVITA), Daudi Maghana, alisema watoto wakipelekwa shule ya viziwi Tabora wamekuwa wakipata elimu nzuri kwa sababu walimu wapo wa kutosha na mashine za kupimia usikivu zipo.