Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 26Article 544267

Dini of Saturday, 26 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali yapokea changamoto za afya, elimu taasisi za dini

Serikali yapokea changamoto za afya, elimu taasisi za dini Serikali yapokea changamoto za afya, elimu taasisi za dini

OMBI la kutafuta suluhisho la changamoto zinazozikabili taasisi za dini zinazotoa huduma za afya na elimu nchini, limepokewa na Rais Samia Suluhu Hassan na ameahidi kuzishughulikia.

Aidha, Rais Samia amezitaka taasisi za dini likiwamo Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) wakati akishughulika na masuala yanayohusu sheria, wao wakae na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) mapema kushughulikia masuala ya elimu ya juu na kuyatatua.

Rais Samia ametoa ahadi hiyo alipozungumza na maaskofu wa TEC, viongozi wa walei, taasisi na mashirika yalio chini ya baraza hilo nchini katika mkutano uliofanyika katika baraza hilo, Kurasini Dar es Salaam, leo.

Amesema hayo baada ya kusikia risala ya baraza iliyosomwa na Rais wa TEC na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya, Gervas Nyaisonga iliyoeleza kuwa mabadiliko ya Sera ya mwaka 2016 yalidhoofisha utoaji wa huduma za elimu na afya kwa taasisi zake ikiwamo kusuasua kwa makubaliano na serikali kwa huduma za afya.

“Tumemsikia Nyaisonga (askofu mkuu), risala imezungumza mengi, kodi kubwa kwa shughuli za kanisa, kodi za umilikishwaji ardhi, kodi za mapato ya ajira, kodi za mapato ya biashara, faini kubwa zinapochelewa kulipwa, kutopata ruzuku ya serikali kwa wakati, ombi la kutaka vyuo vikuu kurejeshewa hadhi ya programu zilizokuwa zinafundishwa.

“Naomba niwahakikishie mengi ni ya kisheria naomba niyapokee nikakae na watu wangu tukayafanyie kazi tuje na suluhu, Mama Suluhu niko hapa, tutafute suluhu kati ya serikali na kanisa tuje na majibu sahihi. Tunaweza kufuta, kupunguza au kutoa msamaha,” alisema. Rais Samia akijibu risala hiyo ya TEC kwake.

Alisema uamuzi wa serikali wa mwaka 2016 kuzuia baadhi ya vyuo kufundisha baadhi ya programu ililenga kulinda ubora wa elimu inayotolewa kwani baadhi vilikuwa havikidhi viwango na upungufu wa wahadhiri ndio maana serikali iliingilia kati.

“Ili turudi kwenye ubora unaotakiwa wanaosimamia vyuo wakae na TCU kuangalia yanayotakiwa na yasiopunguza ubora wa elimu yetu na vyuo hivyo vitafunguliwa,” alielekeza Rais Samia.

Alilipongeza Kanisa Katoliki kwa kugeuza vyuo vikuu kikiwamo Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Cardinali Rugambwa (Carumuco) cha Bukoba na cha Songea kufanya vyuo hivyo kuwa vya ufundi.

Awali, katika hotuba yake alisema alisita kupokea mwaliko akijiuliza atazungumza nini mbele ya maaskofu hao lakini alikumbuka Musa alijitetea kuwa ulimi wake ni mzito si msemaji, lakini Mungu alimwambia aende atampa maneno ya kusema. Rais Samia alisema ametoa habari hiyo ya Musa katika Kitabu cha Biblia Takatifu cha Kutoka 4:12 na kusema: “Nimekubali mwaliko huo kwa sababu hiyo.”

Aliwakumbusha mikakati ya serikali yake kuwa ni kuendeleza mema yote ya awamu zilizopita na kubuni mapya, kukuza uchumi, kuboresha mazingira ya biashara, mapambano dhidi ya rushwa, nidhamu kwa watumishi wa umma na kuendelea kuboresha huduma za jamii, kuendeleza miradi ya kimakakati, demokrasia na uhusiano wa kimataifa.

Aliahidi kuendelea kulinda Katiba kwa kutoa uhuru wa kuabudu kupitia Ibara ya 19 (1) inayotoa uhuru huo na kuimarisha umoja wa kitaifa.

Awali, Rais wa TEC, Askofu Mkuu Nyaisonga alitoa pongezi za baraza hilo kwa kupokea majukumu ya urais kama mwanamke wa kwanza na namna alivyoweza kulivusha taifa kutoka awamu ya tano na kuingia ya sita ya uongozi kwa amani na vita dhidi ya corona, utawala bora na haki za binadamu.