Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 18Article 552073

Habari Kuu of Wednesday, 18 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali yasitisha machinjio ya Punda

Serikali yasitisha machinjio ya Punda Serikali yasitisha machinjio ya Punda

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imeyafungia kwa muda machinjio ya punda yaliyoko Ibadakuli katika Manispaa ya Shinyanga, kutokana na kutoridhishwa na jinsi yanavyoendeshwa na hali ya usafi.

Wizara imesema uchunguzi zaidi wa suala zima la machinjio hiyo utafanywa na kikosi maalumu kitakachopelekwa Shinyanga na kwamba ikibidi machinjio hayo yatafungiwa moja kwa moja.

Katika barua iliyosainiwa na Dk B.L.Malinda kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, imeelezwa kwamba kuna mapungufu mengi kuanzia upakiaji, usafirishaji wa punda kwenye malori kwa umbali mrefu huku wakipata majeraha, hadi namna ya kuchinja ambayo haizingatii haki za mifugo.

Wizara imeeleza kwamba imefuta ruhusa kwa Fang Hua Investment Co. Limited iliyotumiwa barua hiyo wiki iliyopita iliyotolewa Aprili mwaka huu, lakini tangu wiki iliyopita, kampuni imezuiwa kuingiza punda zaidi kwenye machinjio, bali kumaliza wale tu waliokuwa tayari ndani ya eneo lao.

Wizara imeeleza kwamba uchunguzi ukikamilika utatoa msingi wa uamuzi wa mwisho juu ya machinjio hayo yanayodaiwa kuchinja idadi kubwa zaidi ya iliyokubaliwa kwa siku punda 20. Timu ilikuwa ipelekwe pia kusimamia hatua za usitishaji wa uchinjwaji wa punda huko.

Timu za awali za wizara za ukaguzi kwenye machinjio hayo ziliwasilisha wizarani taarifa zinazoonesha kwamba operesheni kwenye machinjio hayo haziendi kwa mujibu wa maagizo yaliyokubaliwa na pande mbili hizo.

Daktari wa Mifugo anayesimamia machinjio hayo, Dk Isaya Gabriel alisema jana kwamba maelekezo ya barua hiyo yalipokewa na kutekelezwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kutetea Haki za Mifugo Arusha (ASPA), Livingstone Masija alipongeza uamuzi huo wa serikali na kuomba ikiwa inawezekana uchinjaji wa punda upigwe marufuku moja kwa moja.

Masija alitoa sababu za rai yake kuwa punda ni rasilimali muhimu kwa kazi kama ubebaji mizigo na ukokotaji wa matela, hasa kwenye jamii za wafugaji na kwenye mikoa yenye ukame.

Alisema kwamba wakati punda mmoja huuza Sh 200,000 tu, kwa siku mnyama huyo akifanya kazi humwingizia mmiliki kati ya Sh 20,000 na Sh 50,000, kima ambacho ni kikubwa na kingemzalishia kiasi kikubwa cha fedha kwa wiki, mwezi na mwaka.

Ruhusa iliyotolewa na wizara katika kuchinja punda ilikuwa na masharti kadhaa, yakiwemo kampuni kusaidia kuwezesha kuanzishwa kwa mashamba binafsi ya kimkataba ya uzalishaji wa punda kuanzia 2018, jambo ambalo halijafanywa.

Masharti mengine ni kila kampuni kuanzisha programu 50 za uhamilishaji kwa kutumia mbegu kutoka koo safu zenye sifa hitajiwa kuanzia Desemba 2018. Ilikubaliwa pia kampuni zenyewe kuanzisha mashamba yake ya kitovu cha kuzalisha punda mwaka huo huo.

Kampuni ilitakiwa kuwa na punda 250 Agosti 2018 na 683 ifikapo mwisho wa mwaka wa nne; kuagiza majike 50 ya koo safu zenye sifa tajwa kutoka China kwa ajili ya kuzalisha punda zaidi na kufanya utafiti wa idadi ya punda katika halmashauri zote zilizopewa ruhusa ya kuchinja mnyama huyo.