Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 18Article 572425

Habari Kuu of Thursday, 18 November 2021

Chanzo: Habrileo

Serikali yataja mikakati bandari ya Bagamoyo

Serikali yataja mikakati bandari ya Bagamoyo Serikali yataja mikakati bandari ya Bagamoyo

SERIKALI imesema hivi karibuni itaanza mazungumzo na wawekezaji wa Bandari ya Bagamoyo ili kuendeleza eneo kwa ajili ya kujenga bandari, eneo la viwanda na eneo la masuala ya usafiri na usafirishaji.

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji, Geoffrey Mwambe, jijini Dar es Salaam.

Mwambe, alisema Kampuni za China Merchants Holdings (International) Co. Ltd (CMHI) na Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA) ambayo awali ilikuwa ikijulikana kama Mfuko wa Uwekezaji wa Serikali ya Oman (SGRF) zitazungumza na serikali.

Alisema majadiliano yatahusu uendelezaji wa eneo dogo la hekta 3,000 kati ya hekta zote 9,800 za mradi mzima wa eneo maalumu la kiuchumi Bagamoyo (BSEZ).

Mwambe alisema miradi inayotarajiwa kujengwa kwenye eneo hilo ni pamoja na Bandari ya Bagamoyo, eneo la viwanda na eneo la usafiri na usafirishaji.

“Tumefanya uchambuzi wa nyaraka zote muhimu, kwa hiyo mazungumzo yataanza karibuni kati ya Serikali na zile pande mbili ambazo ni Kampuni za China Merchants Holdings (International) Co. Ltd (CMHI) na Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA),”alisema Mwambe.

Kwa mujibu wa Mwambe, inakadiriwa thamani ya uwekezaji katika eneo la bandari na kituo cha usafirishaji kufikia Dola za Marekani milioni 3,100 wakati eneo la viwanda thamani ya uwekezaji wake unakadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 2,100 na gharama za ujenzi wa miundominu wezeshi zinakadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 1,400.

Pia aliwataka watu wanaomiliki maeneo kwa ajili ya kujenga viwanda kwenye eneo la hekta 9,800 wawasiliane na serikali wakionesha kusudio la kujenga viwanda hivyo ili maeneo yao yaingizwe kwenye mpango huo kabambe wa uendelezaji wa eneo hilo.

Mwambe alisema mradi wa Bagamoyo ni wa serikali na kwamba kampuni ya China na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman ndiyo waliofanya usanifu (design) na ndiyo watakaojenga na uendeshaji ili warudishe gharama za ujenzi na kisha kuukabidhi kwa serikali.

“Kwa hiyo taasisi hizi mbili ya China na ya Oman watakuja na fedha, teknolojia na menejimenti, na sisi serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) tutaingia pia kwa sababu bandari imelipia fidia lile eneo. Tutakuwa na kampuni ya ubia itakayosimamia mradi ule kati ya taasisi hizi mbili na TPA,”alisema Mwambe.

Mwambe alisema hata madai kwamba Wachina walitaka isiendelezwe bandari yoyote kutoka Mtwara mpaka Tanga si ya kweli bali walichoomba Wachina ni kwamba kutoka Dar es Salaam mpaka Pangani pasiendelezwe bandari kama inayotaka kujengwa Bagamoyo kwa sababu hawatapata faida kutokana na uwekezaji watakaoufanya ambao ni zaidi ya Dola bilioni 10.

Alisema hata madai ya kuwa watauendesha mradi huo kwa miaka 99 si ya kweli ila suala hilo litaamuliwa na mfumo wa hesabu za kiuchumi.

Bandari ya uvuvi

Mwambe alisema Bandari ya Uvuvi iliyotakiwa kujengwa Bagamoyo itajengwa Kilwa ili kutenganisha bidhaa za vyakula na bidhaa nyingine zitakazohudumiwa na Bandari ya Bagamoyo.