Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 18Article 552058

Habari Kuu of Wednesday, 18 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali yataka mpangokazi utekelezaji ahadi za Rais

Serikali yataka mpangokazi utekelezaji ahadi za Rais Serikali yataka mpangokazi utekelezaji ahadi za Rais

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amewaagiza mawaziri na sekretarieti za mikoa watoe taarifa kuhusu ahadi za Rais alizotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu na ziwekewe mpangokazi wa kuzitekeleza.

Alitoa wakati akizindua Mfumo wa Kieletroniki wa Uratibu na Ufuatiliaji wa Shughuli za Serikali (Dashboard), mjini Dodoma jana.

Alisema mfumo huo utaweka uwajibikaji kwa watendaji wa serikali katika kutekeleza ahadi alizotoa Rais wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

"Mfumo huu ni kama fimbo ya kimya kimya ya kutunyoosha na kuwajibika kwa sababu eneo la taarifa na kuwa na takwimu sahihi limekuwa na changamoto kubwa sana," alisema Mhagama.

Alisema wakati wa kuandaa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/2030, serikali haitatumia taarifa nje ya zilizoingizwa katika mfumo huo.

Aliziagiza wizara zitekeleze maagizo na maelekezo ya viongozi wakuu wa kitaifa waliyoyatoa popote walikokuwa na akazitaka zipeleke taarifa za utekelezaji kwa wakati kuhusu maagizo na maelekezo hayo.

Jenista aliwataja viongozi hao kuwa ni Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.

Pia aliagiza taarifa za kazi za mpango mkakati katika vipaumbele kwa kila wizara kwa mwaka huu wa fedha 2021/22 ziwasilishwe haraka.

"Viashiria vya sasa haviko vizuri na katika eneo hili ndio ambalo nitalifuatilia kwa karibu," alisema.

Aidha, aliagiza taarifa za sekta mbalimbali mikoani zikiwemo za kilimo, afya au madini au miradi yoyote zioane na zilizopo katika wizara husika ili zitumike kuandaa taarifa za serikali.

Jenista pia amezitaka wizara ambazo sera zake zimepitwa na wakati wazihusishe ili ziendane na hali ya sasa.

"Hakikisheni kila sera inawekewa mkakati wa utekelezaji wake na muda wa utekelezaji kwa kuzingatia mazingira na mahitaji yaliyopo," alisema.

Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Tixino Nzunda alisema mfumo huo ulianza kutumika mwaka 2017 ukiwa na moduli mbili na sasa umekuwa na moduli tano ambazo ni taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM katika wizara na mikoa, sera, maagizo ya viongozi wakuu wa kitaifa ya Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, ahadi za Rais wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na utendaji wa wizara.

Nzunda alisema lengo la mfumo huo ni kuwezesha upatikanaji wa taarifa za utekelezaji kwa wakati, kuwa sehemu moja ya kupata taarifa na takwimu sahihi kuhusu utendaji wa serikali.