Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 30Article 540607

xxxxxxxxxxx of Sunday, 30 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali yawa mbogo kudhibiti ubadhirifu

SERIKALI ya Awamu ya Sita imeshika kasi ya kufuatilia utendaji miongoni mwa watendaji na watumishi wa umma inayokwenda sanjari na kusimamisha baadhi wanaotuhumiwa kufanya ufujaji wa fedha za serikali hatua ambayo imepongezwa na watu wa kada tofauti.

HabariLeo imebaini katika kipindi cha Aprili hadi Mei mwaka huu kasi hiyo ya wateule wa Rais Samia Suluhu wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa takribani watendaji 40 wametumbuliwa na mawaziri pamoja na Rais mwenyewe, kupisha uchunguzi kutokana na wahusika kukabiliwa na tuhuma mbalimbali.

Ndani ya miezi mitatu ambayo mawaziri wamegusa sekta mbalimbali wakipambana na ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha za serikali na matumizi mabaya ya ofisi, wasomi wamesema hatua hizo zitaimarisha uwajibikaji serikalini.

Wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye ametumbua watendaji kadhaa, mawaziri pia wameshuhudiwa wakifanya ziara na kusimamisha kazi watumishi na watendaji walio kwenye mamlaka zao kutokana na tuhuma mbalimbali zikiwamo za matumizi mabaya ya fedha.

Juzi, Waziri Mkuu Majaliwa aliwasimamisha kazi Mkaguzi Mkuu, Mkaguzi Msaidizi na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya takribani Sh bilioni 1.5 yanayodaiwa kufanyika ndani ya miezi mitatu kuanzia Machi mwaka huu.

Mawaziri moto

Miongoni mwa mawaziri ambao ziara zao zimekuwa moto kwa watendaji, ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu ambaye amewasimamisha kazi wiki mbili watumishi wanne wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kupisha uchunguzi wa ujenzi wa machinjio ya kisasa ambao umegubikwa na tuhuma za ubadhirifu.

Watumishi waliosimamishwa juzi ni Mchumi Gwakisa Mwakyeba, Mkuu wa Idara ya Mifugo, Tito Kagize, Mhandisi wa Ujenzi, Kasimu Thadei pamoja na Mkuu wa Idara ya Manunuzi, Godfrey Mwangairo.

Aprili 25 mwaka huu, Ummy pia aliwasimamisha wakurugenzi wawili wa Mamlaka za Serikali za mtaa baada ya kupokea malalamiko juu ya mwenendo usiofaa, matumizi mabaya ya madaraka na mwenendo usioridhisha wa usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Nao ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Lusubilo Mwakabibi na wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Nyangi Msemakweli.

Vile vile, Ummy alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Magesa Boniphace kuanzia April 20, mwaka huu kupisha uchunguzi dhidi ya malalamiko ya tuhuma za ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo kutoka kwa wananchi na viongozi mbalimbali akiwamo Mbunge wa Sengerema, Hamisi Tabasamu.

Waziri Ummy pia alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, Anosta Nyamoga kupisha uchunguzi kuanzia Aprili 21 baada ya kupokea malalamiko na tuhuma za ubadhilifu wa fedha za miradi ya maendeleo kutoka vyanzo vingine.

Waziri mwingine, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso Aprili 17, mwaka huu, aliwasimamisha kazi watumishi sita akiwamo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), Tamimu Katakwemba pamoja na Ofisa Maji Bonde la WamiRuvu, Simon Ngonyani kwa tuhuma mbalimbali za matumizi mabaya ya ofisi.

Pamoja na tuhuma nyingine za kiutumishi, Ngonyani anadaiwa kusaini mkataba wa fedha nyingi na wakandarasi bila kushirikisha Wizara na hata bila uwepo wa Katibu Mkuu kinyume na taratibu, huku Ofisa wa Bonde akisimamishwa kwa ukiukaji wa maadili ya utumishi.

Hivi karibuni, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani aliwasimamisha kazi kwa siku 10 Meneja wa Tehama na huduma za biashara wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Lonus Feruzi na Wasaidizi wake Frank Mushi na Idda Njau watoe maelezo kutokana na kujitokeza tatizo katika huduma ya manunuzi ya LUKU kupitia njia za kielektroniki.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alipozungumza na Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme (Tanesco), jijini Dar es Salaam alimuagiza Kalemani kutoishia kuwasimamisha kwa siku hizo bali alitaka wakae pembeni hadi uchunguzi zaidi utakapokamilika.

Mwezi uliopita, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro alimsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Devotha Mdachi kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha pamoja na masuala ya Rasilimali Watu zinazoikabili bodi na kuunda kamati kufuatilia.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, John Mtega alikabidhi taarifa hiyo juzi kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ndumbaro pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Allan Kijazi .

Majaliwa

Ndani ya mwezi huu, Waziri Mkuu, Majaliwa amesimamisha watumishi zaidi ya 10 wakiwamo Mkaguzi Mkuu, Mkaguzi Msaidizi pamoja na watendaji saba wa Wizara ya Fedha na Mipango kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma zinazowakabili. Wanadaiwa kujipatia posho takribani bilioni moja kwa kufanyakazi ambazo ni sehemu ya kazi zao.

Wengine waliosimamishwa na Majaliwa Mei 22,mwaka huu ni watumishi watatu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa Sh milioni 780 zinazotokana na zabuni. Waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Huduma Saidizi, Hans Lyimo, Kaimu Mhasibu Mkuu, Jonas Bakuza na Lecian Mgeta aliyekuwa Mhasibu wa wakala.

Mwezi uliopita, Majaliwa alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Suzana Chaula baada ya kutoridhishwa na utendaji wake na kuhusu kuhusu Mtendaji Mkuu wa wakala, Ronald Rwakatare, alikabidhi kwa Mamlaka ya uteuzi ambaye ni Rais.

Uteuzi aliofanya Rais Samia Mei 15, alimteua Dk Edwin Paul Mhede kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa wakala huo.

Rais Samia

Siku 11 tangu alipoapishwa kuwa Rais baada ya kifo cha Dk John Magufuli, Rais Samia alimsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA), Deusdedit Kakoko, kupisha uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha bandarini.

Mei 3, Rais alitengua uteuzi wa viongozi watatu na kuvunja Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania. Alitengua pia uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) Profesa Tadeo Andrew Satta, ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM). Alitengua uteuzi wa wajumbe sita wa bodi ya TASAC.

Wengi wapongeza

Wakizungumzia kasi hiyo ya viongozi wa serikali, watu wa kada tofauti wakiwamo wasomi, wamesema hatua hiyo ni nzuri inayostahili kupongezwa kwani inaongeza imani ya Watanzania kwa serikali yao.

Mtumishi wa Umma wa muda mrefu aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Balozi Ammi Mpungwe alisema kuwa hatua ya kuwashughulikia watendaji wazembe na wabadhirifu inayoendelea kuchukuliwa na viongozi wa serikali itasaidia kuimarisha uwajibikaji serikalini.

Alisema, wananchi wanashauku ya kuona maendeeo na tena kuona miradi ya kimaendeleo ikikamilika kwa uharaka na ufanisi na siyo kusikia wakiibiwa fedha zao. Alisema kama hatua kali zikiendelea kuchukuliwa itasaidia kudhibiti wizi katika fedha za umma hasa ikizingatiwa kuwa wizi huo ni mwiba wa maendeleo.

“Naona hatua ambazo mawaziri wameanza kuzichukua dhidi ya wanaohusika na ubadhirifu ni nzuri zinazotakiwa kupongezwa, tumesikia Waziri Mkuu juzi akiagiza kusimamishwa kazi kwa watendaji Wizara ya Fedha, ni hatua zinazoongeza imani ya watanzania kwa serikali yao.”alisema Balozi Mpungwe.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja alisisitiza umuhimu wa maadili kwa watendaji wa serikali wenye dhamana ya kusimamia nafasi mbalimbali za utendaji.

Alisema kwa kuwa maadili yameahirisha masuala yote yanayopaswa na yasiyopaswa kufanywa na mtumishi wa umma hivyo ni vema watumishi hao kuzingatia zaidi maelekezo ya utumishi wa umma kwa kutojiingiza kwenye matatizo.

Alisema uamuzi wa serikali wa kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wazembe kwenye uwajibikaji ni uamuzi mzuri kwa kuwa inawakumbusha wengine wenye mawazo maovu ya kushiriki kwenye ubadhirifu au kufanya matendo mengine ambayo ni kinyume na maadili kuacha mara moja.

Habari hii imeandikwa na Halima Mlacha na Evance Ng’ingo.

Join our Newsletter