Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 20Article 552808

Habari Kuu of Friday, 20 August 2021

Chanzo: Mwananchi

Serikali yawaonya mabalozi wanaohudhuria kesi ya Mbowe

Serikali yawaonya mabalozi wanaohudhuria kesi ya Mbowe Serikali yawaonya mabalozi wanaohudhuria kesi ya Mbowe

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amewataka mabalozi wanaokwenda mahakamani kufuatilia mwenendo ya kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kufuata sheria na taratibu za kidiplomasia.

Balozi Mulamula ameyasema hayo leo Ijumaa Agosti 20,2021 jijini Dar es Salaama wakati akizungumza na mabalozi, wakuu wa taasisi na mashirika ya kimataifa mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) uliofanyika Lilongwe, Malawi Agosti 17–18.

Katika mkutano huo, Balozi Mulamula amesisitiza kwamba mabalozi wanaokwenda mahakamani kufuatilia mwenendo wa kesi ya Mbowe kufuata sheria na taratibu za kimataifa za kidiplomasia ili kujiepusha na ukiukwaji wa sheria na taratibu hizo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mulamula amesema Serikali haina lengo la kuwazuia mabalozi hao kwenda mahakamani.

Hata hivyo, taarifa hiyo imesema kutokana na uwepo wa janga la Uviko-19 pamoja na msongamano ni muhimu kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kufuatilia shauri hilo kwa njia nyingine ikiwemo kupitia vyombo vya habari.

“Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ndiyo yenye jukumu la kuhakikisha usalama wa wanadiplomasia waliopo hapa nchini. Hata hivyo, kwa siku za hivi karibuni baadhi ya wanadiplomasia hao wameonekana mahakamani bila kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia masuala ya Kidiplomasia ikiwemo kutoa taarifa kwa Wizara ya Mambo ya Nje,” amesema Balozi Mulamula katika taarifa hiyo.

Kwa upande wake, kiongozi wa mabalozi waliopo hapa nchini, Dk Ahamada El Badaoui alisema ulinzi wa mabalozi waliopo hapa nchini ni muhimu na endapo kuna mabalozi wanafanya hivyo ni vyema wakafuata taratibu na sheria zilizopo.

Akizungumza na gazeti hili, mjumbe wa Umoja wa Ulaya hapa nchini ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema wamepokea tahadhari kutoka serikalini kwa wanadiplomasia.

“Tulihudhuria usikilizwaji wa kesi inayomkabili kiongozi wa chama cha upinzani, Freeman Mbowe kwa sababu ni haki yetu kama mabalozi kufuatilia hali ya kisiasa katika nchi ambayo tumo wakati huo.”