Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 26Article 574120

Uhalifu & Adhabu of Friday, 26 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Shahidi adai picha za CCTV zimemvuruga kesi ya Sabaya

Shahidi adai picha za CCTV zimemvuruga kesi ya Sabaya Shahidi adai picha za CCTV zimemvuruga kesi ya Sabaya

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imelazimika kuahirisha kuendelea kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita baada ya shahidi wa 10, Francis Mrosso kudai kuwa anajisikia vibaya.

Shahidi huyo wa Jamhuri, jana alipomaliza kuongozwa kutoa ushahidi wake na Mawakili Waandamizi wa Serikali, Tarsila Gervas na Felix Kwetukia aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi leo.

Shahidi huyo alidai kuwa hali yake siyo nzuri na hajisikii vizuri baada ya kuona video clips sita zikionyesha matukio mbalimbali ya Januari 22, 2021 akiwa Benki ya CRDB tawi la KwaMromboo, Arusha alipoenda kutoa Sh90 milioni.

Ikiwa leo ni siku ya tatu tangu aanze kutoa ushahidi wake kuanzia Novemba 22, 2021 shahidi huyo jana alimalizia ushahidi wake ambapo mahakamani hapo iliwekwa flash yenye clip sita kutoka Benki hiyo, zikimwonyesha namna alivyokwenda kutoa fedha hizo akiwa na baadhi ya watuhumiwa wenzake Sabaya.

Mrosso, ambaye ni mmiliki wa gereji ya Mrosso Injector Pump Service jana alionekana kuwa kimya wakati video hizo zikionyeshwa kwa vipande mahakamani hapo.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Patricia Kisinda anayesikiliza kesi hiyo, shahidi huyo alipomaliza kuongozwa kutoa ushahidi wake aliiomba mahakama impe muda atoke nje kwa dakika chache kabla ya kurejea kuanza kuhojiwa na mawakili wa utetezi, ombi ambalo mahakama iliridhia.

Baada ya kurejea ndani ya chumba cha mahakama hiyo, Mrosso alimuomba Hakimu aahirishe kesi hiyo hadi leo kwa kuwa hajisikii vizuri baada ya kuona matukio hayo kutoka kwenye CCTV Camera yaliyoonyeshwa mahakamani hapo.

Mara baada ya ombi hilo, wakili wa utetezi, Mosses Mahuna alidai haoni sababu ya msingi ya shahidi kutaka apumzike.

Naye Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofmed Mtenga aliomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa shahidi hayuko sawa baada ya kuona video hizo za Januari 22, 2021.

Hakimu Kisinda aliridhia ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 29, mwaka huu ambapo shahidi huyo ataanza kuhojiwa na mawakili wa utetezi.

Awali akiongozwa na mawakili hao, shahidi huyo kupitia video hizo aliwatambua washtakiwa Enock Mnkeni, John Aweyo na Jackson Macha walioonekana katika matukio tofauti ya video hiyo.

Shahidi huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa alilazimika kutoa kiasi hicho cha fedha kwa Sabaya na vijana wake kwani walimtishia kumfungulia kesi ya uhujumu uchumi ama kumpoteza.

“Hizo fedha nilizotoa kwa kulazimishwa ili nisifunguliwe kesi ya uhujumu uchumi na walisema kwa midomo yao akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Hai kuwa nisipotoa feha hizo watanipoteza,”alidai Mrosso.

Awali mahakama hiyo ilitupilia mbali pingamizi lililowasilishwa na mawakili wa utetezi wakipinga kupokelewa kwa nyaraka nne ambazo ni leseni ya biashara,TIN namba na nyaraka mbili za usajili wa kampuni ya Mrosso Injector Pump Service baada ya kujiridhisha zimekidhi matakwa ya kisheria.

Akitoa uamuzi huo mdogo Hakimu huyo alisema baada ya mahakama kupitia hoja za pande zote mbili ameona nyaraka hizo zimekidhi matakwa ya kisheria ikiwemo nyaraka mbili za usajili wa kampuni kuwa nakala halisi.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano ambapo kati ya hayo Sabaya peke yake anakabiliwa na makosa matatu,makosa wanayodaiwa kuyatenda Januari 22,2021 jijini Arusha