Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 26Article 544273

Habari za Mikoani of Saturday, 26 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Shamba la mikorosho la Waziri Mkuu lawa darasa tamu

Shamba la mikorosho la Waziri Mkuu lawa darasa tamu Shamba la mikorosho la Waziri Mkuu lawa darasa tamu

SHAMBA la mikorosho la Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa ambaye pia ni Waziri Mkuu, limetumiwa kuwezesha mafunzo kwa maofi sa ugani, wapuliziaji na watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika wa kuuza mazao(Amcos).

Mafunzo hayo ya matumizi sahihi na salama ya viuatilifu vya kupambana na magonjwa ya mikorosho yanatolewa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari) Naliendele na Bodi ya Korosho nchini.

Mafunzo hayo ambayo yanakusudiwa kutolewa maeneo mbalimbali yanayolima korosho yamelenga kuongeza uzalishaji toka tani laki mbili za sasa hadi tani laki tatu na kuendelea kwa kuwezesha mti mmoja wa mkorosho kutoa kilo 30 za korosho na kuendelea.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ruangwa mkoani Lindi, Andrew Chikongwe alisema kwamba yamefika wakati muafaka, muda ambao wakulima wanapaswa kubadilika.

Alisema eneo la mafunzo limekidhi haja ya kila mkulima kuona ukweli wa kilimo bora na utunzaji wa shamba la mikorosho kwa jinsi shamba la mbunge wao linavyopendeza.

“Tunatakiwa kubadilika kama tunataka kuendelea katika kilimo hiki na wanaoweza kubadilisha hali hii ni washiriki wa mafunzo haya kwa kuambukiza walichojifunza kwa wenzao,” alisema mwenyekiti huyo.

Aidha Chikongwe alitaka elimu ya kilimo kufikishwa hadi kwa wanafunzi mashuleni ili watambue uthamani wa kilimo badala ya hali ya sasa ambao wanafunzi wanaandaliwa kwa kazi za maofisini.

Aliwataka watu wa TARI na Bodi ya Korosho kuhakikisha kwamba mafunzo yanayotolewa yanaendelea kuwabadilisha wakulima ili tija ionekane.

“Kupitia mafunzo haya naamini tubadilisha ya watu wetu na kuwa na uhakika wa kilimo cha korosho na kipato chake” alisema.

Alisema maofisa ugani walioshiriki mafunzo hayo, wapuliziaji na viongozi wa Amcos watawajibika kusambaza elimu hiyo kwa kutengeneza utaratibu maalumu kwa kila mkulima kunufaika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Ruangwa Frank Chonya alisema pamoja na ukweli kuwa shamba la mbunge linafaa kutumika kwa ajili ya mafunzo, wao kama wilaya wameanzisha shamba la ekari 2,000 la mikorosho kulitumia kwa ajili ya shamba darasa na pia kuingiza kipato kwa halmashauri.

Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Ruangwa, Damian Kilevile alisema kwamba mafunzo hayo yanasaidia kuleta udhibiti katika kilimo hicho na kuwa na uhakika kwa kukihudumia kwa utaratibu unaotakiwa ili kuongeza tija.

Zaintuni Manzi ambaye ni Ofisa Kilimo, kijiji cha Nandagala alisema kwamba amefurahishwa sana na mbunge wao kuruhusu shamba lake kutumika kama shamba darasa.

“Hili shamba ni zuri unaonma jinsi lilivyopandwa na kuhudumiwa hilio jdilo shamba la kutumika kuelimisha wakulima wengine,” alisema Zaituni.

Ofisa Uhaulishaji teknolojia na uhusiano wa TARI, Stella Andrea alisema mafunzo hayo yamesukwa kwa kiasi ya kwamba wanawafunza wakulima kuanzia uoteshaji wa mikorosho, utunzaji hadi kipindi cha kuiandaa kwa ajili ya maua , mabibo na korosho zenyewe.

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kwamba kila mkorosho unatoa kilo zaidi ya 30 za korosho na hivyo kuleta tija kwa mkulima.

Miongoni mwa wapuliziaji mikorosho Issa Bakari kutoka kijiji cha Chimbira B alisema amefurahishwa na mafunzo hayo ambayo yamemrekebisha katika elimu ya uchangaji wa dawa na upuliziaji.