Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 24Article 544018

Habari Kuu of Thursday, 24 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Sheria 22 zarekebishwa kuongeza mapato

Sheria 22 zarekebishwa kuongeza mapato Sheria 22 zarekebishwa kuongeza mapato

SERIKALI imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2021 wenye lengo la kufanyia marekebisho sheria 22 ikiwamo ya kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira (PAYE) kutoka asilimia tisa hadi asilimia nane.

Pia imeondoa pendekezo la kutoza kodi mapato kwa asilimia tatu ya mapato ghafi kwa wachimbaji wa madini wadogo na kuweka adhabu ya kiasi cha Sh 500,000 kwa kila mwezi kwa mwajiri aliyeajiri raia wa kigeni na kuchelewa au kushindwa kuwasilisha ritani za kila mwezi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, mabadiliko hayo yamelenga kuboresha taratibu za ulipaji na ukusanyaji kodi, kudhibiti mapato na matumizi ya baadhi ya taasisi za serikali na kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara na uwekezaji ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na hivyo kuongeza mapato ya serikali.

Akifafanua, Dk Mwigulu alisema katika Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332 pamoja na mambo mengine, pia itapunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia tisa hadi asilimia nane.

Alisema pia serikali imeondoa pendekezo la kutoza kodi ya mapato kwa asilimia tatu ya mapato ghafi kwa wachimbaji wa madini wadogo ili kutoa fursa ya kufanya utafiti zaidi kuhusu namna bora ya kuwatoza kodi wachimbaji hawa bila kuathiri ukusanyaji wa mapato mengine.

“Marekebisho haya ni kuwezesha utekelezaji wa kisheria wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 niliyoiwasilisha bungeni Juni 10, mwaka huu. Sheria zinazorekebishwa zinahusu kodi, ushuru na tozo kwa lengo la kurekebisha viwango vya kodi, ushuru, ada na tozo mbalimbali,” alieleza.

Kuhusu Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura 41, Dk Mwigulu alisema imelenga kupunguza kiwango cha kodi kwenye zawadi ya ushindi kutoka asilimia 20 hadi 15 kwenye michezo ya kubahatisha ya ubashiri wa matokeo ya michezo.

“Pia kutoza kodi ya michezo ya kubahatisha kwa asilimia 10 ya mapato ghafi kwenye michezo ya kubahatisha inayoendeshwa kwa kompyuta na michezo ya kubahatisha iliyo chini ya majaribio,” alisema na kuongeza kuwa pia inapendekeza kufuta pendelezo lililotolewa kwenye hotuba ya Bajeti la kuongeza kiwango cha kodi katika michezo ya kubahatisha ya ubashiri wa matokeo ya michezo kwa mapato ghafi kutoka asilimia 25 ya mauzo ghafi hadi asilimia 30 ya mauzo ghafi.

“Hata hivyo pamoja na pendekezo hili, bado asilimia tano kwenye kodi hii itawasilishwa kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Michezo kwa ajili ya kuendeleza michezo nchini,” alibainisha.

Kuhusu Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Sura 178, alisema marekebisho yamelenga kuweka masharti kwa bodi kutoweka ada au tozo yoyote ikiwemo tozo ya thamani ya mkopo kwenye mikopo ya wanafunzi kabla ya kupata idhini ya waziri mwenye dhamana ya elimu baada ya mashauriano na waziri mwenye dhamana ya fedha.

“Hatua hii ina lengo la kuzuia utozaji holela wa ada kwenye mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na kuwapunguzia mzigo wa ulipaji wa mikopo husika,” alieleza.

Alisema Sheria ya Kodi ya Majengo Sura 289 imelenga kutoza kodi ya majengo kwa kila mwezi kwa kiwango cha Sh 1,000 kwa nyumba za kawaida zenye mita moja na Sh 5,000 kwa ghorofa au ‘apartment’ zenye mita moja.

“Ukusanyaji wa kodi hii utafanywa na Tanesco kupitia ununuzi wa umeme, kwa nyumba ambazo hazitumii umeme wa Tanesco, kodi hiyo itakusanywa kwa utaratibu unaotumika sasa,” alisema na kueleza kuwa pia imeweka utaratibu wa kurejesha asilimia 15 ya makusanyo ya kodi ya majengo kwa Halmashauri au Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Kuhusu Sheria ya Kodi ya Usajili wa Magari Sura 124, alisema imelenga kupunguza ada ya usajili wa magari kwa namba binafsi kutoka Sh milioni 10 hadi Sh milioni tano kila baada ya miaka mitatu.

Akizungumzia Sheria ya Mifumo ya Malipo Sura 437, alisema kimeongezwa kifungu kipya 46A ili kuweka tozo katika kila muamala wa kutuma au kutoa fedha kwa kiasi kitakachotofautiana kulingana na thamani ya muamala wa fedha itakayotumwa au kutolewa.

“Pendekezo hili linalenga kutoza tozo ya shilingi 10 hadi shilingi 10,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa, kiasi cha tozo kinatofautiana kulingana na thamani ya muamala wa fedha unaotumwa au kutolewa,” alieleza.

Alisema Sheria ya Udhibiti wa Ajira kwa Raia wa Kigeni Sura 436 inaweka adhabu ya Sh 500,000 kwa kila mwezi kwa mwajiri aliyeajiri raia wa kigeni na kuchelewa au kushindwa kuwasilisha ritani za kila mwezi zenye taarifa za raia wa kigeni aliowaajiri ikiwemo taarifa zao za mishahara kwa Kamishna wa Kazi. Lengo alisema ni kuhimiza uwajibikaji wa hiari.

Alisema mabadiliko ya Sheria ya Bandari Sura 166, Sheria ya Wakala wa Meli (TASAC) Sura 415 na Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Sura 172, yameweka sharti kwa mapato ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), TCRA na TASAC kuingizwa kwenye akaunti maalumu zitakazofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania.

“Aidha, taasisi hizi zitapatiwa fedha kulingana na bajeti iliyoidhinishwa na baada ya kupata ridhaa ya Mlipaji Mkuu wa Serikali,” alieleza.

Alisema Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta Sura 220 inaelekeza fedha zitakazokusanywa kutokana na ongezeko la ushuru wa barabara na mafuta la Sh 100 kwa aina zote za mafuta kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA).

Alisema pia kuongeza ushuru wa barabara kwa Sh 100 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli.

Alisema Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Sura 82 pamoja na mambo mengine inapendekeza kufuta Tozo ya Elimu na mafunzo ya Ufundi Stadi kwa hospitali zinazomilikiwa na taasisi za kidini.