Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 06Article 541264

Habari za Mikoani of Sunday, 6 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Sikonge yavunja kamati ya ukusanyaji mapato

Sikonge yavunja kamati ya ukusanyaji mapato Sikonge yavunja kamati ya ukusanyaji mapato

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora limevunja kamati inayoshughulikia ukusanyaji mapato baada ya kutoridhishwa na kasi yao.

Akifafanua juu ya uamuzi huo baada ya kikao cha Baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni, Mwenyekiti wa Halmashauri, Rashid Magope alisema madiwani hawajafurahishwa na utendaji wa kamati hiyo.

Alisema kasi ndogo ya utendaji wa timu hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Ofisa wa Mapato, Rose Mistika imesababisha halmashauri kushindwa kupata mapato ya kutosha katika kata zote ikiwamo ambazo zimekuwa zikifanya vizuri.

Alisema kata mama ya halmashauri yenye vyanzo vingi vya mapato na iliyokuwa ikifanya vizuri, chini ya timu hiyo imeshindwa kufikisha nusu ya lengo, kwani wamekusanya asilimia 37 kati ya Januari na Machi.

“Bado tuko chini sana kwenye mapato na kwa kasi hii hatuwezi kufikia lengo, tumemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri aiondoe Kamati yote na kuweka watu wengine,” alisema.

Magope alisisitiza kuwa kila mtumishi anapaswa kubadilika kiutendaji ili kwenda na kasi ya serikali vinginevyo hawatafumbia macho uzembe unaoashiria kurudisha nyuma maendeleo ya halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Andrea Masanja ambaye ni Diwani wa Kata ya Nyahua, alisema kuwa hadi sasa ni kata chache zilizofikia lengo la mapato. “Hii imesababishwa na timu hiyo kushindwa kusimamia zoezi hilo ipasavyo.”

“Tumeshauri timu nzima ya mapato ibadilishwe ili halmashauri yetu iweze kufanya vizuri, tunataka kila mtaalamu awajibike ipasavyo kwenye eneo lake na yule anayezembea tumwondoe mara moja,” alisema.

Diwani wa Kata ya Ipole, John Mbogo alibainisha kuwa serikali ilishaagiza kila halmashauri kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato na kwamba ambayo haitafikia lengo la mapato ivunjwe, hivyo mtumishi yeyote atakayebainika kukwamisha zoezi la ukusanyaji mapato hawatamfumbia macho.

Join our Newsletter