Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 03Article 545107

Habari Kuu of Saturday, 3 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Siku 100 za Rais Samia: Dola milioni 425 za elimu zapatikana

Siku 100 za Rais Samia: Dola milioni 425 za elimu zapatikana Siku 100 za Rais Samia: Dola milioni 425 za elimu zapatikana

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema mafanikio makubwa ya Rais Samia Suluhu katika elimu kwa siku 100 ni pamoja na kuwezesha kupatikana Dola za Marekani milioni 425 (Sh bilioni 927) kwa ajili ya kuendeleza elimu ya juu.

Akizungumza katika kipindi maalumu kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuhusu siku 100 za uongozi wa Rais Samia, Profesa Ndalichako alisema fedha hizo zitafanya mambo makubwa katika kuboresha miundombinu ya elimu ya juu katika vyuo vyote vya serikali nchini.

Alisema maboresho hayo ni pamoja na ujenzi wa kampasi ya kufundisha masuala ya afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili eneo la Mloganzila kama kilivyo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kilichopo Muhimbili, Upanga ambapo Sh bilioni 103 zimetengwa.

Profesa Ndalichako alisema Chuo Kikuu cha Kilimo cha Butiama pia kitajengwa kwa fedha hizo kama ilivyokusudiwa na zitajenga pia Shule Kuu ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Waziri Ndalichako alisema maabara ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) itaboreshwa huku wakitekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kukuza na kuboresha mashamba darasa.

“Hivyo katika kipindi chake (Rais Samia) tuna mradi ambao tunatekeleza wa kuimarisha elimu ya sekondari ambapo kupitia mradi huo tunategemea kujenga shule 1,026 ambapo kati ya shule hizo 26 ni maalum kwa wasichana za bweni kuwapunguzia adha ya kwenda na kurudi nyumbani. Hakika Kazi Inaendelea katika Wizara ya Elimu,” alisema Profesa Ndalichako.