Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 18Article 552064

Habari Kuu of Wednesday, 18 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Simbachawene kuhusu Magereza kujitegemea

Waziri Simbachawene Waziri Simbachawene

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kujenga vitega uchumi, kuimarisha uzalishaji wa bidhaa na utoaji huduma bora katika magereza mbalimbali nchini.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi katika Kituo cha Biashara cha Isanga, Simbachawene aliwapongeza viongozi wa jeshi hilo na wanajeshi kwa juhudi zao za kujiondoa kuitegemea serikali kuu katika mahitaji yao.

“Chapeni kazi, songeni mbele katika kujenga vitega uchumi na kuwekeza, historia itawakumbuka,” alisema.

Simbachawene aliwataka kusonga mbele katika kuleta maendeleo kwa kujenga na kutekeleza miradi mbalimbali na kujenga vitega uchumi katika magereza nchini.

Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania, Kamishna Jenerali, Selemani Mzee alisema kwa sasa Magereza katika nchi nzima kuna kazi ama za kilimo, ufundi au ujenzi wa vitega uchumi na shughuli nyingine za maendeleo, hivyo akamwomba Waziri Simbachawene asichoke ataalikwa mara nyingi ama kuweka jiwe la msingi au kuzindua.

Kamishina Jenerali Mzee alisema ujenzi wa Kituo cha biashara cha Isanga kama kitega uchumi cha jeshi hilo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutaka jeshi hilo lijitegemee.

Akisoma risala ya ujenzi wa Kituo cha Biashara cha Isanga, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Kenneth Mwambije alisema ujenzi wa kituo hicho hadi kukamilika kwake utatumia Sh milioni 550.

Mwambije alisema kituo hicho kitakuwa chanzo cha mapato katika Magereza na kitatoa fursa kwa wakazi wa Dodoma kuwekeza.

Kituo hicho kitakuwa na fremu za biashara, maeneo ya maduka makubwa, sehemu ya mapumziko na vyumba vya kuonesha bidhaa mbalimbali.

Pia kitakuwa na kumbi mbalimbali za starehe, kitakuwa na maeneo ya michezo kwa watoto, maeneo ya kuosha magari, maeneo ya kufanyia mazoezi, nyumba za wageni, jiko pamoja na eneo la kupatia chakula.