Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 16Article 542929

Habari Kuu of Wednesday, 16 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Sumaye, Warioba wamlilia Baregu

Sumaye, Warioba wamlilia Baregu Sumaye, Warioba wamlilia Baregu

MAWAZIRI wakuu wastaafu Frederick Sumaye na Joseph Warioba wamemzungumzia Profesa Mwesiga Baregu aliyefariki dunia Jumapili kuwa alikuwa mwanasiasa hodari aliye mfano wa kuigwa na wengine.

Walieleza hayo jana walipozungumza na HabariLEO walipokwenda kuhani msiba nyumbani kwake Kunduchi, Dar es Salaam.

Profesa Baregu alifariki dunia saa 5:00 usiku wa kuamkia Jumapili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Mwili wake utaagwa keshokutwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Kunduchi Beach, kisha kusafirishwa kwenda mkoani Kagera kwa maziko yatakayofanyika Jumapili kijijini kwake Maruku, Bukoba Vijijini.

Wakati wa uhai wake, Profesa Baregu aliwahi kuwa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), baadaye alisitishiwa mkataba kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kuchanganya utumishi na siasa, hivyo akahamia Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT).

Sumaye amemwelezea Profesa Baregu kuwa ni kati ya wanasiasa waliokuwa wakifanya zaidi kazi zao za siasa kwa weledi na umakini wa hali ya juu.

Alisema alikuwa ni mwalimu na mlezi aliyetumia usomi wake kuchagiza mabadiliko katika medani za siasa nchini.

“Alikuwa anajua kazi yake na alikuwa akitumia weledi wake kupigania maendeleo ya siasa na mambo mengine mazuri, alikuwa anajua anachokifanya, hakika ameacha pengo,” alisema Sumaye.

Naye Jaji Warioba alisema Profesa Baregu alikuwa mwanasiasa aliyechagiza maendeleo kwa asilimia kubwa.

Alisema alikuwa anapenda mijadala endelevu iliyokuwa na tija kwa jamii na taifa zima kwa ujumla na kuwataka wanasiasa wengine kuutambua na kuuenzi mchango wake kwa kufanya kazi.

Profesa Baregu aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Tangu amefariki dunia kila siku kumekuwa kukifanyika misa jioni nyumbani kwake na kesho mwili utapelekwa kulala nyumbani kwake na Ijumaa utapelekwa kanisani KKKT Kunduchi Beach kwa ajili ya ibada ya kumuaga tayari kwa safari ya kwenda kuzikwa Kagera Jumapili. Ameacha mjane na watoto sita.