Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 19Article 543394

Habari za Afya of Saturday, 19 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAA yafadhili hospitali ya kivule

TAA yafadhili hospitali ya kivule TAA yafadhili hospitali ya kivule

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imekabidhi vifaa mbalimbali vya afya kwa ajili ya Hospitali ya Kivule iliyopo katika wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa TAA katika wiki ya maadhimisho ya Utumishi wa Umma.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa Uongozi wa Hospitali jana kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Pamela Mugarula alisema msaada huo umetolewa ukiwa na lengo la kumsaidia mama na mtoto.

“Kwa kidogo ambacho tulichokipata tumeamua tukitumie kuwavusha hawa wakina mama na watoto wachanga kwani ikumbukwe kuwa Serikali mwaka 2018 ilizindua kampeni ambayo ilikuwa na lengo la kupunguza vifo vilivyotokana na uzazi na kuhakikisha mama na mtoto wanakuwa salama,” alisema.

Alisema, “ katika maadhimisho haya ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Mamlaka imeamua kujisogeza karibu na jamii iliyo karibu na viwanja vyetu vya ndege, na ndio maana tukachagua Kivule ambapo kuna hospitali kubwabaada ya kusikia Kivule ina hospitali kubwa hivyo tukaona wanastahili kupata msaada huu ili kupunguza japo kidogo baadhi ya vifaa watakavyovihitaji katika hospital hiyo.”

Katika maadhimisho hayo ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo huanza Juni 16 hadi 23, kila mwaka, Mamlaka hiyo hujikita katika kusaidia jamii mbalimbali kwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali kama; mashuka, barakoa, dawa za kusafishia vyoo, vifaa vya ofisi, glavu , vitakasa mikono, mashine za kuhifadhi vitakasa mikono, mafagio na sabuni za kunawa mikono.

Kiongozi huyo alisema kuwa msaada huo kila mwaka na mwaka huu umelenga kusaidia hospitali haswa katika huduma zinazotolewa kwa mama na mtoto ili waweze kujikinga na maambukizi mbalimbali na kwamba wataendelea kutoka msaada huo kadri itakavyowezekana.

Awali akitoa taarifa ya hospitali hiyo Mganga Mfawidhi, Dk Thobias Nyamboto alisema hospitali hiyo inahudumia wakazi wapatao 700,000 wa Manispaa ya Ilala na Wilaya za jirani za Temeke na Kisarawe.

“Hospitali hii imeanza kutoa huduma Juni 2020 na kwasasa inahudumia wagonjwa wapatao 150 kwa siku ikiwemo wajawazito 50 na tangu kuanza kwa hospitali hii imeweza kuhudumia wagonjwa takribani elfu 24 na wajawazito 708 waliojifungua," alisema Dk Nyamboto.