Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 21Article 573265

Habari Kuu of Sunday, 21 November 2021

Chanzo: mwananchidigital

TANESCO mtegoni tatizo la umeme

TANESCO  mtegoni tatizo la umeme TANESCO mtegoni tatizo la umeme

. Wakati Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) likiendelea na mikakati yake liliyoieleza ya kukabiliana na mgao wa umeme unaonukia, wadau wameshauri juu ya umuhimu wa kuwa na vyanzo tofauti vya nishati hiyo muhimu, ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza pindi uzalishaji wa chanzo kimoja unapolega.

Mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini, John Heche alisema Tanzania inahitaji kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo tofauti, ikiwamo nishati jadidifu, badala ya kujikita katika chanzo kimoja cha maji ambacho muda wowote uzalishaji wake unaweza kupungua.

“Serikali inapaswa kujikita katika vyanzo vingine vya umeme. Kiongozi aliyepita alijikita kwenye miradi ya uwekezaji mkubwa ambayo inachukua muda mrefu na kugharimu fedha nyingi. Kuna haja ya kuwa na uwekezaji wa kati wa miradi ya umeme wa upepo, jua na jotoardhi ambavyo vyote ni vyanzo vya nishati safi,” alisema Heche katika moja ya mjadala katika jukwaa la kimtandao la clubhouse.

Hoja yake haikutofautiana na ya Waziri wa zamani wa nishati, Profesa Sospeter Muhongo, aliyelieleza Mwananchi kuwa umeme uliopo nchini ni mdogo, na Tanzania inahitaji zaidi ya megawati 10,000 kwa miaka mitano ijayo, kwa ajili ya kufanikisha matumizi yake ya ndani na kuuza nje ya nchi, kama ilivyopanga kulingana na vyanzo ilivyonavyo.

“Kila siku nasikia mnaimba suala la umeme wa maji, lakini mtu anayejua masuala ya umeme, umeme wa maji kukupatia faida ni lazima uwe umewekeza fedha nyingi na inahitaji miaka mingi kurejesha gharama za uwekezaji ili umeme uwe wa bei nafuu,’ alisema Profesa Muhongo .

Alisema umeme wa maji bei yake haipungui baada ya kumaliza ujenzi wa bwawa, isipokuwa kwa mtu ambaye hataki kurudisha fedha za uwekezaji.

Alisema ni muhimu kuwa na mchanganyiko wa vyanzo vya uzalishaji wa nishati, kwa kuwa kuna matarajio kuwa bara la Afrika linaweza kukumbwa na ukame, hivyo kama njia ya kujiandaa na hali hiyo, alisema ni vyema kukawa na uzalishaji wa umeme unaotokana na maji, gesi asili, upepo, jua, jotoardhi na bayomasi.

Wakati ambapo mabadiliko ya hali ya hewa yanatajwa kama sababu ya kuwapo kwa mgawo wa umeme unaonukia, mchangiaji aliyejitambulisha kwa jina la Allen Kimambo, alisema katika mjadala wa club house kuwa mabadiliko ya hali ya hewa ni kitu kinachotabirika, hivyo kunapaswa kuwa na mipango ya mapema ya kukabiliana na athari hizo.

“Tunahitaji kuwa na vyanzo mbadala kama vile matumizi ya nishati ya gesi na vinginevyo. Tanzania ina miradi ambayo haijakamilika kama ilivyopangwa, kutokana na hali hiyo tunapaswa kuwa na mpango wa dharura,” alisema Kimambo.

Kwa upande wake Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kuna haja ya kufanya mapitio ya kisheria, ili kuruhusu mtu yeyote kuomba leseni ya kuzalisha na kusambaza umeme kwa watu.

“Serikali inapaswa kusimamia miundombinu ya usambazaji pekee na kubaki kuwa msambazaji mkuu. Hata hivyo, baadhi ya maeneo yanatakiwa kuwa huria, kama sheria inavyoelekeza,” alisema Zitto.

Zitto alisema utekelezaji wa sheria zinazosimamia umeme ziliwekwa kando miaka mitano iliyopita, akitolea mfano sheria ya umeme ya mwaka 2008 na kusema kuwa Serikali inachopaswa kufanya kwa sasa ni kutekeleza sheria.

Aidha, alizungumza umuhimu wa kuwekeza kwenye gesi na nishati jadidifu, akisema suluhu ya kudumu ya tatizo la umeme ni utekelezaji wa mpango wa kutatua changamoto za nishati wa mwaka 2016 (power system masterplan).

Wazungumzia mgawo

Wakati hofu ikiwa ni kuwapo kwa mgawo wa umeme, baadhi ya wadau na watumiaji walitaka kuwapo kwa mfumo mzuri wa upatikanaji wa nishati hiyo wakati wa mgawo.

Mtaalamu wa uchumi, Profesa Samweli Wangwe alisema katika mgawo, maeneo muhimu katika uchumi yapewe kipaumbele ili kutoathiri uchumi wa mtu mmojammoja na wa nchi kwa jumla.

“Kinachotokea ni fundisho kuwa umeme wa maji si wa kutegemewa hususani wakati huu ambapo kumekuwa na mabadiliko ya tabia ya nchi. Serikali iliyopita ilielekeza nguvu kubwa huko, lakini nguvu hiyo ingepelekwa kwenye gesi tungekuwa mbali sana,” alisema Profesa Wangwe huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na vyanzo vingi vya kuzalisha umeme.

Mjasiriamali Ayoub Kawambwa wa jijini Dar es Salaam, alitoa wito kwa Tanesco kuwa na upendeleo katika mgawo wa umeme akisema kipaumbele kiwe kwa maeneo ya viwanda na maeneo mengine yanayohitaji umeme wa mara kwa mara.

Alisema maeneo hayo yenye viwanda, yanatoa fursa za kiuchumi kwa watu wengi husuani wenye kipato duni, hivyo hivyo athari za umeme katika maeneo ya viwanda zinaweza kuathiri maisha yao.

“Tunahitaji pia kuwa na ufumbuzi wa muda mfupi na mrefu wa upungufu wa nishati. Hii inapaswa kwenda sambamba na uwekezaji zaidi kwenye matumizi ya gesi kwa kuwa tayari kuna miradi inayolenga kutumia na kusambaza gesi,” alisema Kawambwa.

Mkurugenzi wa sera na uchechemuzi wa shirikisho la wenye viwanda nchini (CTI) Akida Mnyenyelwa, ili kutoathiri uzalishaji viwandani, maeneo yenye viwanda yanapaswa kuendelea kuwa na umeme wa kutosha muda wote.

Alisema katika mazingira ya kutokuwa na umeme, wazalishaji hutumia gharama kubwa kwa ajili ya jenereta ambazo husababisha kuongezeka kwa gharama za uzalishaji.

Alisema hata hivyo, jenereta ni rahisi kuzitumia kwa viwanda vidogo na sio vile vikubwa.

“Kutumia jenereta kuendesha kiwanda kikubwa ni ghali sana, jambo hilo huongeza gharama za uzalishani na kuzifanya bidhaa za kiwanda husika kutokuwa shindani sokoni,” alisema Mnyenyelwa.