Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 22Article 558997

Habari Kuu of Wednesday, 22 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

TANESCO yatenga Tsh. Bilioni 122 kusambaza umeme

TANESCO yatenga Tsh. Bilioni 122 kusambaza umeme TANESCO yatenga Tsh. Bilioni 122 kusambaza umeme

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limetenga bajeti ya ndani ya Sh bilioni 122 kwa ajili ya vifaa vya kuunganishia wateja umeme.

Meneja Mwandamizi wa Tanesco Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Hassan Said alisema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza kwenye Kipindi cha Power Breakfast kilichorushwa jana na Kituo cha Televisheni cha Clouds.

Katika kipindi hicho ,wananchi walituma ujumbe mfupi wa maneno wakiuliza kuhusu huduma za Tanesco huku wengi wakilalamika kulipia gharama za kuunganishiwa umeme kwa muda mrefu bila kuunganishiwa huduma hiyo.

Baadhi ya wananchi walidai kuwa wamelipia huduma hiyo ya kuunganishiwa umeme kwa zaidi ya miezi minne hadi sita lakini kila wakiuliza wanaambiwa vifaa kama nyaya, nguzo na mita havipo.

“Hilo la wateja kucheleweshwa kuunganishiwa umeme linatokana na uhaba wa vifaa, lakini tumejipanga na bajeti yetu ya ndani tumeongeza shilingi bilioni 122 kwa ajili ya wateja zaidi ya 300,000 wanaotakiwa kuunganishiwa umeme wale waliolipia,”alisema Said.

Aliongeza, “Tumejipanga, fedha hizo zitatumika kuondoa kero hizo zote kwa wateja zaidi ya 300,000 waliokwishalipia na bado hawajaunganishiwa huduma, lengo letu ni kuhakikisha wateja wanapata huduma bora.”

Alisema wanaboresha miundombinu ya usambazaji umeme kwa kujenga mfumo wa umeme wa mzunguko ili itokeapo tatizo kwenye laini moja, umeme ukatwe laini husika badala ya kukata laini zote kama ilivyo kwa sasa.

Said alisema kero ya kukatika umeme mara kwa mara katika maeneo tofauti haitokani na uhaba wa nishati hiyo isipokuwa changamoto za mifumo ya usambazaji na wakati mwingine kwa sababu ya maboresho.

Meneja huyo mwandamizi wa Tanesco alisema, maboresho mengine yanayoendelea kufanywa na shirika ni kuweka nyaya za umeme chini ya ardhi badala ya kupitisha juu.