Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 15Article 557692

Habari za Afya of Wednesday, 15 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

TMDA yataja njia nne za kutengeneza chanjo ya corona 

TMDA yataja njia nne za kutengeneza chanjo ya corona  TMDA yataja njia nne za kutengeneza chanjo ya corona 

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imesema hadi sasa ziko njia nne za kutengeneza chanjo za virusi vya corona (COVID-19 ambazo zimegunduliwa na kuanza kutumika duniani ambazo zimethibitishwa na Shirika la Afya Duniani(WHO) .

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo katika taarifa yake aliyotoa mwishoni mwa wiki kuhusu maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu corona, alisema hadi sasa njia nne za kutengeneza chanjo za corona ndio zimethibitishwa na WHO kutengeneza chanjo.

Alitaja njia hizo nne kuwa zile chanjo ambazo hutengenezwa kwa kutumia virusi vya corona vilivyoondolewa makali au kudhoofishwa hivyo kujenga kinga kwenye mwili wa mtumiaji.

Aina ya pili ni zile chanjo zilizotengenezwa kwa protini ambazo hutumia vipande protini visivyo na madhara au ganda la protini ambalo hufanana na virusi vya corona ili kutoa kinga ya mwili.

Aina ya tatu ni chanjo za vekta za virusi ambazo hutumia virusi salama visivyoweza kusababisha magonjwa lakini hutumika kama sehemu ya kutengenezea protini za virusi vya corona ili kutoa kinga.

Mfano wa chanjo hizo na ambazo zimedhibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ni Janssen ya Kampuni ya Johnson & Johnson ambayo Tanzania imepokea dozi milioni 1.5 kupitia Mpango kimataifa wa WHO wa kusambaza Chanjo kwa nchi masikini (Covax).

Aina ya nne ni chanjo zitokanazo na vinasaba (RNA na DNA) na hutumia RNA au DNA iliyoundwa na vinasaba kutoa protini ambayo husababisha kinga ya mwili na mfano wa chanjo hizo ni kama Pfizer–BioNTech na Moderna ambazo zimeidhinishwa WHO.

Taarifa ya TMDA, ilisema chanjo ya Janssen inayotumika sasa nchini kudhibiti corona, imethibitishwa na kuidhinishwa kuwa miongoni mwa chanjo tano nchini zinazotumika kukinga corona.

Chanjo hizo tano zilizoidhinishwa na serikali ya Tanzania baada ya kufanyiwa uchunguzi na mamlaka za TMDA, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR),Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii na mamlaka nyingine ni Janssen,Pfizer,Moderna,Sinopharm na Sinovac.

“TMDA huidhinisha chanjo ambazo zimependekezwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutumika nchini. Chanjo ambazo sasa zinaruhusiwa kutumika nchini Tanzania ni pamoja na Janseen,Pfizer, Moderna ,Sinopharm na Sinovac,”alisema Fimbo Mkurugenzi wa TMDA.

Wakati TMDA wakisema hayo, watafiti na wataalamu na washauri wa afya wa WHO,wametoa mapendekezo ya matumizi ya chanjo ya Janssen katika mapambano dhidi ya corona na kusema ni moja ya chanjo zinazosaidia kukinga na kupunguza madhara ya corona kwa kiasi kikubwa.

Katika taarifa rasmi za WHO mtandaoni, Chanjo ya Janssen imetengenezwa na vekta za virusi salama visivyoweza kusababisha magonjwa na kiasi cha chanjo inayotolewa kwa mtu ni mililita 0.5 (mls) na huchomwa dozi moja tu kwenye msuli.

WHO inasema chanjo hiyo ni salama na kama zilivyo dawa nyingine inaweza kuwa na madhara madogomadogo kama kuumwa kichwa, kichefuchefu, mwili kuchoka, homa lakini maudhi hayo hupotea ndani ya siku chache.

Hata hivyo chanjo ya Janssen imetajwa kuwa salama na yenye ufanisi mzuri hata kwa watu wenye maradhi sugu, kama matatizo ya moyo, saratani ,sukari, matatizo ya figo,mapafu,presha, wenye umri zaidi ya miaka 50.

Kuhusu muda wa chanjo kuanza kufanya kazi, WHO inasema mara baada ya mtu kuchanjwa, kinga huanza kujitengeneza na hadi ndani ya siku 14 mwili huwa umetengeneza kinga ya kutosha kupambana na adui.

Hata hivyo, utafiti uliofanywa kuhusu chanjo ya Janssen umeonesha kuwa siku 28 baada ya mtu kuchanjwa mwili wake ulitengeneza kinga ya kupambana na corona kwa kati kwa asilimia 85.4 na asilimia 93.1 ya waliopata chanjo hawakufikia hatua ya kulazwa hospitalini.

Kuhusu tahadhari ya kuchomwa chanjo, WHO inashauri watu wenye joto la mwili linalozidi nyuzi joto 38.5 wasichomwe chanjo kwanza hadi pale joto litakaposhuka na kwamba wale wote wenye umri chini ya miaka 18 hawaruhusiwi kuchomwa chanjo hiyo ya Jansseen .

Sababu za kutochomwa chanjo hiyo ya Janssen kwa mujibu wa taarifa kutoka Kampuni ya Johnson&Johnson ambao ndio watengenezaji wa chanjo hiyo ni kuwa wakati wa utafiti wa chanjo, watu wenye miaka 18-0 hawakufanyiwa utafiti kwa chanjo hiyo.

Wataalamu hao wa afya wameshauri kuwa ni vyema mtu aliyechanjwa akaendelea kuchukua tahadhari zote dhidi ya corona na kwamba hata kama akipata maambukizi, madhara yake ni madogo na anaweza kupona bila hata kutumia dawa au kulazwa hospitalini.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Muungano wa taasisi za kimataifa za kutoa chanjo mbalimbali(GAVI),inasema chanjo ya Janssen ni moja ya chanjo zilizofanyia majaribio na kuonesha ufanisi wake wa kupambana na corona na hivyo kuthibishwa na kuidhinishwa kutumika.

Moja ya faida ya chanjo hiyo ni uhifadhi wake ni rahisi na wenye masharti nafuu hivyo inaweza kusambazwa mataifa mengi duniani kusaidia kupambana na janga la corona.

Taarifa za mtengenezaji wa chanjo hiyo Kampuni ya Johnson& Johnson, chanjo cha Janssen inahifadhiwa kwenye baridi ya nyuzi joto kati ya 2 hadi 9 hivyo inaweza kusafirishwa kwa kuhifadhiwa kwenye majokofu yenye kiwango hicho cha baridi kwa mataifa mengi duniani.