Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 04Article 540943

xxxxxxxxxxx ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

TRA yapeleka watalaamu elimu ya mlipa kodi Kigoma 

KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata ameongoza timu ya watalaamu wilayani Kasulu, mkoani Kigoma, kwa ajili ya kutoa elimu na huduma kwa walipa kodi.

Akizungumza na wafanyabiashara katika wilaya hiyo, Kidata alisisitiza umuhimu wa kila upande, yaani wafanyabiashara na watumishi wa TRA kuzingatia haki na wajibu wao kila wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

"Sisi watumishi wa TRA tunafanya kazi kwa kufuata misingi yetu ya maadili ambayo ni uwajibikaji, uadilifu na weledi lakini pia kama mmoja wenu alivyosema ni lazima pia sote, ninyi na sisi TRA tuzingatie haki na wajibu kila tunapotekeleza majukumu yetu," alisema.

Alisema timu hiyo ya watalaamu wa elimu kwa mlipakodi watakaa wilayani humo kwa wiki nzima wakipita duka kwa duka wakitoa elimu ya kodi na kutatua haraka changamoto za kikodi zinazowakabili wafanyabiashara hususani makadirio ya kodi.

"Nimepokea maoni, ushauri na changamoto zenu na mimi kwa kulitambua hili nimekuja na timu ya watalaamu kutoka TRA Makao Makuu ambao nitawaacha hapa kwa ajili ya kuwaelimisha sheria na taratibu za ulipaji kodi ikiwa ni pamoja na haki na wajibu wenu. Pia, watamsikiliza kila mfanyabiashara mwenye changamoto na kuzitatua," alisema.

Aidha, Kamishna Mkuu huyo alizungumza na watumishi wa TRA wa Mkoa wa Kigoma na kuwataka kuzingatia kufanya kazi kwa bidii na weledi ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati na hiari huku wakiwapatia elimu ya kodi.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) wilayani Kasulu, Prosper Guga alisema wamefurahishwa na kitendo cha viongozi wa TRA kufika wilayani hapo na kufanya nao mazungumzo pamoja na kupeleka timu ya watalaamu kutoa elimu kwa walipakodi hao kwa lengo la kutatua changamoto zilizojitokeza.

Hivi karibuni, wafanyabiashara wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma walifanya mgomo na kufunga maduka wakidai kuwa watumishi wa TRA wilayani humo hawana lugha nzuri na wanawakadiria makadirio makubwa, hali waliodai inasababisha washindwe kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.

Join our Newsletter