Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 03Article 540775

xxxxxxxxxxx of Thursday, 3 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

TRILIONI 1.4/ZATENGWA UMEME BWAWA LA NYERERE

SERIKALI imetenga Sh trilioni 1.4 kwa ajili ya kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2021/ 2022 katika mradi wa kimkakati wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere Hydro Power Project (JNHPP).

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, aliyasema jana bungeni Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Alisema katika mwaka 2021/22, serikali itaendelea na utekelezaji wa mradi huo na kwamba, kazi zitakazofanyika ni pamoja na kuendelea kukamilisha ujenzi wa bwawa, ujenzi wa njia kuu za kupitisha maji, ujenzi wa kituo cha kuzalishia umeme na ujenzi wa kituo cha kusafirisha umeme.

Ujenzi wa mradi huo ulianza Juni, 2019 na unatarajiwa kukamilika Juni, 2022.

Kalemani alisema mradi huo ukikamilika, pamoja na miradi mingine, hadi mwaka 2025 Tanzania itakuwa na jumla ya takribani Megawati 5,000.

Alisema serikali imeendelea na utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati na wa kielelezo wa JNHPP utakaozalisha megawati 2,115 kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji.

Kwa mujibu wa Kalemani, gharama za mradi huo ni Sh trilioni 6.55 zinazotolewa na serikali kwa asilimia 100.

Alisema katika mwaka 2020/21, kazi zilizofanyika ni pamoja na kukamilisha uchimbaji na ujenzi wa handaki la kuchepusha maji ya Mto Rufiji, kuendelea na ujenzi wa bwawa, ujenzi wa njia kuu za kupitisha maji, ujenzi wa kituo cha kuzalishia umeme na ujenzi wa kituo cha kusafirisha umeme.

“Hadi kufikia mwezi Mei, 2021, jumla ya Shilingi trilioni 2.495 zimelipwa kwa mkandarasi sawa na asilimia 100 ya fedha iliyotakiwa kulipwa kulingana na hatua ya utekelezaji wa mradi iliyofikiwa,” alisema Dk Kalemani.

Alisema kwa jumla utekelezaji wa mradi katika maeneo muhimu matano hadi kufikia Mei mwaka huu, umefikia wastani wa asilimia 52.

“Hadi sasa jumla ya wafanyakazi 7,243 wameajiriwa. Kati ya wafanyakazi hao, 6,452 ni Watanzania sawa na asilimia 89.1 na kutoka nje ya nchi ni 791 sawa na asilimia 10.9,” alisema Dk Kalemani.

Kuhusu mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi I Extension – MW 185, alisema unahusu upanuzi wa Kituo cha Kinyerezi I – MW 150 kwa kujenga mitambo itakayozalisha MW 185 na hivyo, kufanya kituo kuzalisha jumla ya MW 335.

“Mradi huu unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 188 sawa na takriban Sh

bilioni 435.48. Kwa ujumla, utekelezaji wa mradi hadi sasa umefikia asilimia 84,” alisema.

Akaongeza; “Hata hivyo, kutokana na mkandarasi (M/s Jacobsen Elektro AS ya Norway) aliyepewa kazi hiyo kushindwa kutekeleza mradi ipasavyo, taratibu za kumpata mkandarasi mpya wa kumalizia kazi zipo katika hatua za mwisho.”

Kalemani alisema fedha za ndani Sh bilioni 88.58 zimetengwa katika mwaka 2021/22 kwa ajili ya kukamilisha utekelezaji wa mradi huo na kwamba, ujenzi unatarajiwa kuanza Julai mwaka huu na utakamilika Mei, 2022.

Join our Newsletter