Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 03Article 555205

Habari Kuu of Friday, 3 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa kuhusu kutokea ukame na joto kali Tanzania

Taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa kuhusu kutokea ukame na joto kali Tanzania Taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa kuhusu kutokea ukame na joto kali Tanzania

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua za vuli zinazotarajiwa zitakuwa chini ya wastani na huenda zikasababisha sehemu kubwa ya mikoa inayopata mvua hizo kwa misimu miwili kwa mwaka kuwa na ukame.

Pia, kutakuwa na vipindi vya joto kali kuliko kawaida katika msimu wa vuli.

Akitabiri mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Oktoba hadi Desemba, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, Dk Hamza Kabelwa alisema mwaka huu zitaanza kwa kusuasua na kuambatana na mtawanyiko usio sawa.

Dk Kabelwa aliitaja mikoa itakayopata mvua ya wastani na chini ya wastani kuwa ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Simiyu, Mara, mashariki mwa Mkoa wa Shinyanga na visiwa vya Unguja, Pemba na Mafia.

Mikoa mingine alisema ni ya kanda ya ziwa, ukiwamo Kagera, Geita, Mwanza na kaskazini mwa Kigoma itakayopata mvua za wastani na chini ya wastani.

“Kutakuwa na upungufu wa mvua katika nchi yetu, hivyo kutajitokeza kunyesha vipindi vifupi vya mvua kubwa ambazo zinaweza kufika kati ya milimita 50 hadi 70 ambazo zinaweza kuleta mafuriko,” alisema Dk Kabelwa.

Alisema upungufu wa unyevu wa udongo unatarajiwa kujitokeza maeneo mengi, hali inayoweza kuathiri ukuaji wa mazao na ongezeko la wadudu washambuliao mazao kama mchwa, viwavijeshi, panya pamoja na magonjwa ya mimea.

Dk Kabelwa ameshauri wakulima kupanda mazao yanayokomaa ndani ya muda mfupi na yanayostahimili ukame na watumie teknolojia za kilimo himilivu kuhifadhi unyevunyevu wa udongo.

Alisema mamlaka husika zinashauriwa kutoa ushauri kwa wakulima juu ya njia bora na namna ya kutumia kiwango kidogo cha mvua kinachotarajiwa kunyesha sambamba na matumizi mazuri ya akiba ya chakula kilichopo.

“Upungufu wa kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini unaweza kupunguza upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali, ukiwamo uzalishaji wa umeme, lakini utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi utaendelea vizuri,” alisema.

Kwa upande wa menejimenti za maafa, zinashauriwa kuwa na usalama wa chakula, malisho ya mifugo, maji na kutoa miongozo ya namna ya kukabiliana na maafa ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Hata hivyo, alisema utabiri wa msimu huu wa vuli unafanana na wa mwaka 2005 ambapo upungufu wa mvua ulisababisha kutokea kwa ukame katika maeneo mengi nchini.