Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 27Article 559819

Habari Kuu of Monday, 27 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Taarifa ya serikali kuhusu tatizo la ukatili kwa wanawake makazini

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi na Ajira), Jenister Mhagama Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi na Ajira), Jenister Mhagama

SERIKALI imevitaka vyama vya wafanyakazi, vya waajiri na taasisi zote kujitathmini upya kwa kuhakikisha vinaweka dhamira ya dhati ya kutokomeza ukatili wa wanawake mahala pa kazi ambao umekithiri.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi na Ajira), Jenister Mhagama, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la wadau kuhusu ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake maeneo ya kazi.

Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) likiwa na kauli mbiu isemayo, ‘Uwajibikaji kutokomeza na udhalilishaji mahali pakazi’ lilikwenda sambamba kwa kufanyika mkutano mkuu wa mwaka.

Waziri Mhagama alisema vitendo vya ukatili wa wanawake mahali pa kazi vinaacha madhara na maumivu makubwa kwa wahanga na jamii inayowazunguka.

“Ninatoa wito kwa wafanyakazi, vyama vya wafanyakazi, vyama vya waajiri na taasisi zote kuwa mstari wa mbele kuonyesha kwamba vimedhamiria kukomesha ukatili wa wanawake mahala pa kazi.

“Hatuwezi kuwa na taasisi hizi imara halafu bado ukatili unaendelea, turudi tukajitathmini wajibu wetu ndani ya vyama hivi kama tunautekeleza vizuri. Lengo la vyama vya wafanyakazi ni kutetea maslahi na ustawi wa wafanyakazi maeneo ya kazi.”

Kwa mujibu wa Mhagama, kama ukatili unaendelea, lazima warudi kuangalia sera na sheria ndani ya vyama hivyo kwa hali iliyopo sasa, kama zinatekeleza au wanatakiwa kufanya mabadiliko yake.

Alisema kwa upande wa sheria za kazi wizara yake ipo tayari kukaa navyo, ili kufanya marekebisho na kupata maeneo ambayo yanaweza kusaidia kufanya vita hiyo iwe rahisi.

“Ipo mikataba ambayo tumeridhia na mingine ambayo bado hatujaridhia hatuna budi kufanya kazi ya kina kuangalia uridhiaji wa mikataba hiyo, utengenezaji sheria zinazohusu mikataba hiyo ili ziendane na mazingira, mila na desturi tulizonazo,” alisema.

Waziri huyo alipongeza hatua iliyofikiwa na WiLAF Tanzania ya kupinga matukio hayo na kuwaeleza kuwa wanastahili kupongezwa na yeye yupo tayari kushirikiana nao.

“Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inatambua na imeamua kuhakikisha inawalinda wanawake dhidi ya ukatili wa kijinsia na tutafanyakazi hiyo kwa nguvu zetu zote.

“Kwenye hili kongamano mmesema ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wenu unaosema wanawake na ajira na lengo ikiwa ni kuboresha mazingira mazuri ili wanawake waweze kushiriki katika shughuli za uchumi wa viwanda ninawapongeza.”

Alisema mradi huo unaendana na dhana nzima ya Rais Samia ambaye ameamua kuwa balozi wa wanawake kwa kutekeleza kwa vitendo usawa wa kijinsia kwa kuona umuhimu wa wanawake kushiriki katika ujenzi wa uchumi.

Alisema Rais Samia amevunja miiko iliyokuwapo tangu uhuru kwa kufanya uteuzi kwenye nafasi ambazo hazijawahi kushikwa na mwanamke akitolea mfano uteuzi wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stegomena Tx.

Mwenyekiti wa WiLDAF, Monica Mhoja, alisema lengo la kongamano hilo ni kujadili ukatili na udhalilishaji wa wanawake katika sekta ya kazi na ajira.

Alisema lengo lingine ni kupendekeza mbinu na kuandaa mpango mkakati wa pamoja katika kuondoa matatizo yaliyopo sehemu za kazi.

Edmund Moshy kutoka Mwakilishi wa Shirika la Kazi Ulimwenguni (ILO), aliiomba serikali kuridhia na kuupitisha mkataba wa 190 unyanyasaji mahali pa kazi ambapo mpaka sasa nchi sita tu ndiyo zimeuridhia.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Anna Bahati, alisema katika kuunga mkono suala hilo chama kilitoa mafunzo ya kuzuia kabisa unyanyasaji mahali pa kazi mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Morogoro ambayo ilikuwa na wawakilishi kutoka Dar es Salaam na Dodoma.