Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 19Article 543388

Dini of Saturday, 19 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Taasisi za kidini zatoa simu janja 300

Taasisi za kidini zatoa simu janja 300 Taasisi za kidini zatoa simu janja 300

TAASISI ya dini ya Kiislamu na Kikristo nchini (TIP) imetoa simu janja 300 kwa vijana wilayani Ilemelea, Buchosa na Kwimba ili kurahisisha utoaji taarifa za ukatili wa kijinsia kwa wakati.

Sambamba na hilo, simu hizo (100 kila Wilaya) zitasaidia pia kutuma jumbe katika mitandao ya kijamii zinazohamasisha upimaji wa virusi vya ukimwi (VVU) , hasa kwa wanaume na watoto chini ya miaka 18.

Kabla ya ugawaji wa simu wiki hii, vijana walipatiwa mafunzo ya namna bora ya kutumia mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe kwa walengwa.

Mkurugenzi wa TIP, Saida Mukhi alisema kila ujumbe wa ukatili wa kijinsia utakaotumwa kwenye mitandao ya kijamii utakua umeunganishwa moja kwa moja na wadau pamoja na taasisi husika ikiwemo dawati la jinsia la polis, Ustawi wa jamii, maendeleo ya Jamii, Wizara ya afya na TIP, kwa hatua za haraka.

“Shughuli hizi mbili za kuhamasisha upimaji VVU na kupinga ukatili wa kijinsia ni sehemu ya mradi wa Boresha tunaoutekeleza katika wilaya hizo tatu. Lengo ni kuwa na jamii ya watu wanaojua hali ya afya zao na uwepo wa usawa,” alisema.

Alisisitiza kwamba mradi wa Boresha ulioanza 2019 na kutarajiwa kuisha mwaka huu umehusisha upimaji wa VVU baada ya tafiti mbalimbali kuonesha mwamko mdogo wa wanaume na watoto.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi, mbali na vituo vya afya TIP imekua ikianzisha vituo vya upimaji katika nyumba mbalimbali za ibada ili kuongeza wigo wa upimaji.

Mratibu wa Ukimwi wilayani Ilemela, Gasper Lugela alisema mradi huo utasaidia katika kuhamasisha kwani muamko kwa watoto/ vijana bado uko chini.

Alisema angalau wale wa umri wa kati ya miaka 25 na 45 wamekua wakijitajidi kupima ispokua wenye miaka kuanzia 15 hadi 24 muamko uko chini.

“Muamko mdogo huenda ni kwasabu wengi wenye umri huo wanakua shuleni ambapo vituo vya kupima ni adimu. Nashauri viwepo vituo mashuleni na mahala pengine ambapo vijana wanakusanyika kwa wingi ikiwemo viwanja vya michezo, na tuwe na utaratibu wa kuwafuata hukohuko,” alisema.