Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 29Article 544624

Habari za Mikoani of Tuesday, 29 June 2021

Chanzo: ippmedia.com

Tabora wampongeza Rais kuimarisha umoja na mshikamano

Tabora wampongeza Rais kuimarisha umoja na mshikamano Tabora wampongeza Rais kuimarisha umoja na mshikamano

Pongezi hizo zimetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk. Batilda Burian, alipokuwa akiongea na Waandishi wa habari ofisini kwake kabla ya kuanza kikao cha wazee na viongozi wa dini.

Amesema katika siku 100 za uongozi wake, Rais Samia amefanikiwa kuunganisha wananchi kuwa kitu kimoja na kuwaondolea hofu baada tu ya kufiwa na aliyekuwa Rais wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli.

Aidha amebainisha kuwa Rais amehamasisha na kuimarisha uhusiano mwema baina ya nchi yetu na nchi jirani na kujenga diplomasia ya kiuchumi na mataifa hayo kupitia ziara zake alizofanya.

‘Tunampongeza Rais wetu kwa kuimarisha uhusiano mwema na nchi jirani, kujenga haki na usawa wa kijinsia, kuanzisha kamati ya kukabiliana na Corona na kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii na kusikiliza kero zao’, alisema.

Pia, amefafanua kuwa Rais amekipa uhuru chombo cha Mahakama katika kufanya maamuzi yake bila kupokea masharti kutoka katika muhimili mwingine wa dola na haki imeendelea kutendeka.

Amesema katika siku 100 za utumishi wake, mapato yameendelea kuongezeka kutokana na hamasa na elimu ya kodi anayotoa na sasa watu wanalipa kodi kwa hiari bila shuruti wala nguvu ya dola, aidha alimpongeza kwa kuja na mbinu mpya zitakazosaidia nchi kupiga hatua kubwa kiuchumi.

Akifafanua baadhi ya mambo ambayo Rais ameufanyia Mkoa huo katika siku 100 za mwanzo, amesema kuwa wamewapewa fedha za kujenga zahanati 40 ambapo kila halmashauri itakuwa na zahanati tano.

Batilda ameongeza kuwa wamepata sh milioni 500 kwa kila jimbo kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mradi wa bomba la mafuta ambazo zitawezesha pia kujengwa kwa karakana na makambi.

Amewashukuru wazee wa mkoa huo kwa kuendelea kuwa chachu ya amani hapa nchini, aliwaomba kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita na kuwa mabalozi wazuri wa amani na maendeleo katika mkoa wao.