Uko hapa: NyumbaniInfos2021 02 25Article 526117

xxxxxxxxxxx of Thursday, 25 February 2021

Chanzo: habarileo.co.tz

Tacaids, NACP wazindua machapisho kuhusu VVU

TUME ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) pamoja na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi Tanzania (NACP) kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kupitia mpango wa Tulonge Afya wamezindua machapisho ya uhamasishaji wanaume na watoto kutumia huduma za virusi vya ukimwi (VVU) kupitia viongozi wa dini nchini.

Uzinduzi wa machapisho hayo unalenga kuwezesha taasisi na viongozi wa dini nchini kuwa na taarifa sahihi kuhusu maambukizi, upimaji na matibabu ya VVU, kuboresha utoaji wa ujumbe mpya kwa waumini ili kuongeza idadi ya waumini hasa wanaume na watoto kupata huduma za VVU na Ukimwi.

Kaulimbiu ya mpango huo ni Chaguo Jipya, Matibabu Mapya, Wakati Mpya, Tumaini Jipya.

Akizungumaza jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa machapisho hayo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk Leonard Maboko, alisema taasisi za dini zina jukumu la kupeleka habari na ujumbe mpya kwa jamii kuhusu huduma zilizorahisishwa za upimaji wa VVU.

Aidha, machapisho hayo yanalenga kutoa elimu kuhusu matibabu na kuibua mijadala inayolenga kuleta mabadiliko chanya dhidi ya tabia hatarishi zinazochochea maambukizi mapya ya VVU.

Tabia hatarishi ni pamoja na vijana kufanya ngono katika umri mdogo, vitendo ya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake na ulevi.

Maboko alitaka jamii kuzingatia matibabu na matumizi sahihi ya dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARVs) ili kupunguza uwezekano wa ongezeko la maambukizi ya VVU.

“Hadi kufikia mwaka 2016/17 kiwango cha maambukizi ya VVU Tanzania Bara kimeshuka kutoka asilimia 5.3 hadi asilimia 4.7 kwa watu wenye umri wa miaka 15 - 49. Pamoja na afua nyingi zilizotekelezwa kupunguza maambukizi mapya nchini, taasisi za dini zimekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio haya,” alisema.

Alisema mkakati uliopo kati ya Tacaids, taasisi za dini nchini na wadau wengine wanaofanya kazi kwenye afua mbalimbali za VVU, ni kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi na hatimaye, kuudhibiti ifikapo mwaka 2030.

Mwakilishi wa USAID, Anathy Thambinagam, alisema viongozi wa dini, taasisi na mashirika ya dini yana nguvu kubwa katika kutoa ujumbe muhimu na hatua za kinga kwa jamii dhidi ya VVU na Ukimwi.

“Wao ni washawishi wakuu na wanaaminiwa sana na waumini, hivyo wanakuwa katika hatua nzuri ya kubadilisha mienendo ya waumini wao…,” alisema.

Mshauri wa USAID Tulonge Afya, Michael Luvanda, alisema uzinduzi huo ni pamoja na ‘Mwongozo wa Ujumbe Mpya wa Tumaini’ kwa Wakristo na Waislamu, kalenda za rasilimali za ibada kwa Waislamu na Wakristo na imani na jamii.

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata), Nuhu Mruma, alisema viongozi wa dini wanatambua kuwa zana hizi zimekuja wakati mwafaka wakati serikali inakusudia kumaliza kuenea kwa VVU ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini katika uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Moses Matonya, alipongeza serikali kwa kutambua mchango wa viongozi wa dini katika kushughulikia changamoto mbalimbali za kijamii.

Join our Newsletter