Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 22Article 573316

Habari Kuu of Monday, 22 November 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Taifa lajivunia umiliki ardhi, fursa za uwekezaji

William Lukuvi, Wazii wa Ardhi William Lukuvi, Wazii wa Ardhi

Katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru, serikali inajivunia kupanga, kupima na kumilikisha wananchi ardhi sanjari na kutengeneza fursa za uwekezaji.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema hayo jana jijini Dodoma wakati akieleza mafanikio na maendeleo ya sekta ya ardhi katika miaka 60 ya Uhuru.

Lukuvi alisema mafanikio hayo yamepatikana katika awamu tofauti za uongozi kwa kutunga, kuboresha na kusimamia sera na sheria ikiwa ni baada ya kuondokana na sera na sheria za kikoloni.

"Katika miaka 60 ya uhuru, tumepanga; tumepima; tumemilikisha; tumewawezesha wananchi kuwa na makazi bora; tumeboresha mifumo; tumetengeneza fursa za uwekezaji; tumeweka mfumo mzuri wa utatuzi wa migogoro na tumesogeza huduma za ardhi karibu kabisa na wananchi."alisema.

Lukuvi alisema serikali imeweza kupanga ardhi katika matumizi mbalimbali, miji imesanifiwa na kuwezesha upatikanaji wa huduma kwa ajili ya ustawi wa jamii katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kimazingira.

"Ili kukabiliana na ongezeko la watu nchini, usanifu wa miji umewezesha kupatikana kwa huduma muhimu kwa wananchi na kukuza uchumi wa nchi."alisema.

Alisema ongezeko la watu nchini limefikia takribani watu 59,441,988 kwa makadirio ya mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 79.7 huku ikikadiriwa idadi ya watu wanaoishi mjini ni sawa asilimia 35 ikiwa ni tofauti na baada ya Uhuru ambapo sensa ya mwaka 1967, Tanzania ilikuwa na watu 12,313,469 ambapo asilimia 5.7 walikuwa wakilishi mjini na asilimia 94.3 walikuwa wakiishi vijijini.

"Ukuaji huu wa idadi ya watu umechagiza mahitaji makubwa ya matumizi ya ardhi iliyopangwa kwa shughuli za makazi, kilimo, ufugaji, miundombinu, uwekezaji na biashara,"alisema Lukuvi.

Alisema tangu uhuru mpaka sasa michoro ya mipangomiji 21,844 yenye idadi ya viwanja 6,784,426 imesanifiwa kwa matumizi yakiwemo makazi, makazi biashara, taasisi, viwanda, maeneo ya huduma za jamii, maeneo ya wazi.

Lukuvi alisema pia maeneo 496 yametangazwa kuwa ya kupangwa , kuendelezwa na kusimamiwa kimji kwa kuzingatia Sheria ya Mipangomiji Sura ya 355.

Alisema makazi 1,992,245 katika maeneo yalioendelezwa kiholela na ambayo yalikuwa ni mtaji mfu kwa wananchi yamerasimishwa na kuwezesha wananchi kuwa rasmi, usalama wa milki zao, na hadhi ya kukopesheka.

Lukuvi alisema katika kutimiza azma ya serikali ya kuwa na ardhi ya uwekezaji, eneo lenye ukubwa wa ekari 885,144 lilitengwa na kumilikishwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali ikiwamo viwanda, kilimo, hoteli na biashara.

Alisema pia ardhi yenye ukubwa wa ekari 224,439.4 imetengwa kwa ajili ya uwekezaji kupitia Mipango Kabambe ya miji, mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya na Vijiji, ardhi iliyomilikishwa kwa wawekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji (EPZA) na ardhi ya akiba.

Lukuvi alisema mafanikio makubwa zaidi yamepatikana katika masuala ya upimaji kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kisasa na usimikaji wa miundombinu ya kisasa ya upimaji yenye kurahisisha upimaji.

Alisema pia kubadili mfumo wa upimaji kutoka Mfumo wa zamani wa Arc 1960 ambao ulikuwa umejengwa juu ya mtandao hafifu wa alama za msingi za upimaji , kwenda mfumo mpya wa kisasa wa TAREF 11 ambao ni mfumo wa kimataifa unaowezesha upimaji kati ya nchi na nchi na wenye alama zenye usahihi wa hali juu.

Lukuvi alisema kutokana na mfumo na vifaa vya kisasa, viwanja 2,783,278 na mashamba 28,784 yamepimwa nchini kote.