Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 03Article 540694

xxxxxxxxxxx ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Takwimu wajaribu vifaa vya sensa

OFISI ya Takwimu ya Taifa (NBS) imefanya majaribio ya vishikwambi na simujanja zitakazotumika wakati wa sensa ya watu na makazi mwakani kuona namna vifaa hivyo vinavyofanya kazi ya kukusanya, kutuma takwimu na taarifa kwenye seva kuu.

Akizungumza katika mitaa ya Kata ya Chang’ombe jijini Dodoma wanakofanyia majaribio, Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi (NBS), Daniel Masolwa, alisema wanafanya majaribio ya vifaa pekee.

Alifafanua kuwa, hiyo si sensa ya majaribio wala si sensa yenyewe, bali ni majaribio ya vifaa hivyo vya kisasa vitakavyotumika wakati katika Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

Masolwa alisema ukiacha majaribio hayo ya vifaa, sensa ya majaribio itafanyika Agosti mwaka huu huku sensa halisi ya watu na makazi ikitarajiwa kufanyika Agosti, 2022.

Alisema kwa sasa wataalamu hao wa takwimu za watu na makazi, wanapima uwezo wa vifaa hivyo vya kidigiti katika maeneo yaliyotengwa kuhusu namna vinavyoweza kutumika katika kukusanya takwimu wakati wa sensa.

Tofauti na sensa nyingine zilizotangulia, mwaka huu takwimu zitakazokusanywa katika maeneo yaliyotengwa ambayo ni mitaa na vitongoji, zitatumwa moja kwa moja kwenye seva katika ofisi za NBS.

Kabla ya kutumwa kwa takwimu hizo, vishikwambi na simu janja zitatakiwa kukusanya na kuzituma kwa mtandao hadi kwenye ofisi za takwimu kwa ajili ya kuchambua na kuzipanga.

Kwa mujibu wa Masolwa, tofauti na miaka iliyopita, takwimu za mwaka huu zitakuwa na uhakika zaidi kutokana na ukweli kwamba, vishikwambi vitakuwa na uwezo wa kurekebisha matokeo kama mtumaji atakuwa amekosea.

“Hakuna uwezekano wa kupikwa takwimu kwa sababu vishikwambi vitafunguka tu kama mkusanyaji atakuwa kwenye eneo ambalo limebainishwa au limewekwa alama, si vinginIlibainika kuwa, faida kubwa ya kutumia teknolojia hiyo ni uhakika wa takwimu na kutumia muda mfupi kupata matokeo kwa kuwa hakuna madodoso ya makarasi na badala yake, taarifa huandikwa moja kwa moja.

Diwani wa Kata ya Chang’ombe jijini Dodoma vinakojaribiwa vifaa vya kukusanyia takwimu, Bakari Fundikira, alipongeza uamuzi wa NBS kufanyia majaribio katika kata yake.

Katika kufanya majaribio hayo ya vifaa ili kuhakikisha vinatoa takwimu sahihi, zaidi ya watumishi 60 kutoka NBS, Tamisemi na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi walishiriki.

Fundikira alisema wamechagua Kata ya Chang’ombe kutokana na ukweli kwamba ndiyo kata yenye wakazi wengi kati ya kata zote 41 za Jiji la Dodoma na watu wake wana maisha ya kawaida.

Alisema kwa kufanyia huko watapata hali halisi ya maisha ya watu, itakuwa rahisi kupanga mipango ya jiji kutokana na ukweli kwamba wananchi wa kata hiyo wana maisha ya kawaida.

Kwa mujibu wa takwimu za 2012, kata hiyo ilikuwa na wakazi 25,415, hivyo kwa kufanya majaribio katika mitaa minne ya kata hiyo watapata takwimu wanazotaka kwa ajili ya serikali kupanga mipango yake.

Join our Newsletter