Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 07Article 541384

Habari Kuu of Monday, 7 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tamisemi: Hakuna tatizo uchaguzi shule, vyuo

Tamisemi: Hakuna tatizo uchaguzi shule, vyuo Tamisemi: Hakuna tatizo uchaguzi shule, vyuo

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imesema hakuna tatizo lililotokea wakati wa upangaji wa shule na vyuo kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2020.

Baadhi ya wazazi walilalamika kwenye mitandao ya kijamii wakidai kuwa upangaji wa tahasusi haukuzingatia sifa za ufaulu za wanafunzi.

Katibu Mkuu wa Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe jana aliwaeleza waandishi wa habari mjini Mtwara kuwa, upangaji huo unafanywa kwa mfumo wa kikompyuta ukizingatia daraja la ufaulu katika tahasusi ambazo mwanafunzi alijaza kupitia fomu ya chaguo la mwanafunzi.

Profesa Shemdoe alisema, mawasiliano hafifu baina ya wazazi na wanafunzi kuhusu tahasusi walizojaza kwenye fomu ya maombi ndiyo yanayosababisha malalamiko hayo kkwa baadhi ya wazazi.

"Wanafunzi walitakiwa kujaza taasusi tano, na shule wanazotaka kwenda kusoma... Mfumo wetu wa upangaji ambao ni wa kielektroniki huchagua wanafunzi kwa kuangalia alama na chaguo lake."

"Niombe wazazi wenzangu pale wanapoona kuna kitu hawaelewi, kuna maofisa elimu wa mikoa na wilaya kwa hiyo ni vema wakawafuata kwa ajili ya kupata ufafanuzi na mfumo huu umekuwa ni mfumo ambao umekuwa na uwazi," alisema.

Naibu Katibu Mkuu kutoka Tamisemi, Gerald Mweli, alisema: "Sisi katika machaguo tunakupanga kutokana na kile ambacho mtoto mwenyewe amekichagua, jambo la pili tunakupanga kweny shule maalumu uliyochagua kulingana na combination (tahsusi) yako."

Mweli alisema watoto wote waliochaguliwa, wamechagua kulingana na hiyo shule aliyoichagua na shule hiyo ikijaa, wanaenda kwenye shule ambayo iko karibu zaidi na halmashauri anayotoka mwanafunzi.

"Kila mwaka tunapopata changamoto, huwa tunaboresha mifumo yetu ya kufanya kazi… Mwaka jana changamoto tuliyoipata ni kulalamika ni kwamba, umewapanga watoto mbali, lakini kuna wazazi ambao walishindwa kuja kuwaleta watoto kwenye shule zenye ufaulu mkubwa," alisema Mweli.

Alisema, mwaka huu mfumo huo ulitengenezwa baada ya kupanga watoto kulingana na ufaulu na zile shule zenye ufaulu mkubwa kujaa na wale watoto wenye ufaulu wa kawaida wanapangwa shule za bweni kutokana na ufaulu wao.

Taarifa ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais-Tamisemi, Nteghenjwa Hosseah, ilieleza juzi kuwa, wanafunzi wote walitakiwa kuweka machaguo matano ya tahasusi za kidato cha tano pamoja na machaguo ya vyuo kwa ambao wangekosa nafasi za kidato cha tano na kwa wale ambao wangependa kwenye vyuo vya kati moja kwa moja.

“Ukweli ni kwamba, wanafunzi wamepangwa kulingana na machaguo yao kulingana na ufaulu na sifa za kuchaguliwa kwenye tahasusi husika,” alisema Hosseah na kuongeza: “Hivyo, kuna wanafunzi wamechaguliwa kujiunga kwenye tahasusi ambayo ni chaguo lake la tano kulingana na ufaulu wake.”

Alisema mwanafunzi aliyekosa machaguo yake kutokana na ushindani unaodhibitiwa na nafasi zilizopo kwa mwaka husika, huchaguliwa kwenye tahasusi nyingine yoyote aliyofaulu huku kipaumbele kikienda kwa tahasusi za sayansi.

Kwa mujibu wa Nteghenjwa, wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na nafasi za vyuo huchaguliwa kwa utaratibu huo huo wa kuzingatia machaguo yao wenyewe na fani nyinginezo ikiwa wamekosa machaguo yao kulingana na nafasi zilizopo.

Join our Newsletter