Uko hapa: NyumbaniHabari2021 10 12Article 562867

Habari Kuu of Tuesday, 12 October 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tamisemi kutoa ‘mkeka’ wa madarasa fedha za IMF

Tamisemi kutoa ‘mkeka’ wa madarasa fedha za IMF Tamisemi kutoa ‘mkeka’ wa madarasa fedha za IMF

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amesema leo atatangaza mgawanyo wa matumizi ya Sh trilioni 1.3 za kukabili athari za janga la Covid-19 kwenye kila mkoa.

Ummy jana alisema leo atatangaza kila mkoa utapata kiasi gani na kila halmashauri itapata mgawo.

Alisema hayo katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuapisha viongozi watatu ambao ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sofia Mjema, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Omari Othman Makungu na Jaji Kiongozi, Mustapha Mohamed Siyani.

“Kesho (leo) tutatoa mkeka wa jinsi gani kila mkoa utapata madarasa mangapi, na tumezingatia vigezo, idadi ya wanafunzi ambao wanatarajiwa kuanza kidato cha kwanza kila halmashauri, kila mkoa na idadi ya watoto ambao wamemaliza kidato cha nne,” alisema Ummy.

Alisema Tamisemi itatenda haki kwa kuzingatia mahitaji ya kila eneo na hakuna halmashauri itakayokosa hata darasa moja.

Ummy alisema viongozi wa Tamisemi wana bahati kwa kuwa juhudi za Rais Samia zimewaondolea changamoto ya kero iliyokuwa ikikabili wananchi ya kulazimishwa kuuza mifugo kwa ajili ya michango ya kujenga madarasa.

“Mheshimiwa Rais umewatua mzigo mkubwa sana Watanzania na hususani wa vijijini,” alisema na kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mjema akasimamie matumizi ya fedha hizo.

Alisema Tangu Julai hadi Septemba mwaka huu, mkoa huo umepata Sh bilioni 5.2 za kujenga zahanati 24, vituo sita vya afya, na hospitali tano za halmashauri.

Juzi wakati Rais Samia Suluhu Hassan anazindua Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alitangaza kuwa fedha hizo zitatumika kwenye sekta mbalimbali ukiwemo ujenzi wa madarasa 15,000 ya sekondari.

Fedha hizo mkopo nafuu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), pia zitatumika katika kujenga madarasa 3,000 ya shule za msingi shikizi, kununua madawati 462,795, kumalizia vyuo vya Veta 32, kununua magari 25 ya kuchimba visima vya maji, na pia kununua mitambo mitano ya kujenga mabwawa ya maji.

Fedha hizo pia zitatumika katika kujenga vyumba vya uangalizi maalumu vya wagonjwa (ICU) 72, kununua magari ya wagonjwa 395 na magari 214 kwa ajili ya kusambaza chanjo.

Pia zitatumika kuweka mifumo ya oksjeni katika hospitali 82, kununua mitungi ya gesi 4,640 kwa ajili ya huduma ya waathirika wa Covid-19, kujenga mitambo 40 ya kuzalisha hewa ya oksigeni na kununua vitanda 2,700 vya wagonjwa.

Pia zitatumika katika kununua mashine za mionzi (X-Ray) za kisasa 85, kununua CT-Scan 29 na pia kuweka mitambo ya MRA katika hospitali zote nchini.